F CCM Manyara yaagiza Miradi isiyokamilika kukamilishwa haraka Mbulu. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

CCM Manyara yaagiza Miradi isiyokamilika kukamilishwa haraka Mbulu.

Na John Walter -Mbulu

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Peter Toima, ameitaka serikali wilayani Mbulu kuhakikisha kuwa miradi yote ambayo bado haijakamilika inamalizwa kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma zilizoahidiwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Toima ametoa agizo hilo wakati akiiongoza Kamati ya Siasa ya CCM ya mkoa wa Manyara katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Mbulu katika Halmashauri zake mbili.

Miradi hiyo inahusisha sekta za elimu, barabara, afya na maji, yenye thamani ya shilingi bilioni 4.6.

Akiwa katika hospitali ya mji wa Mbulu, Toima amesisitiza umuhimu wa kuwapa kazi wakandarasi wenye uaminifu na dhamira ya dhati, badala ya kuwategemea wakandarasi "wababaishaji" wanaoshindwa kutekeleza makubaliano ya mikataba.

“Haina maana kuwapa kazi wakandarasi wanaokiuka makubaliano; wapewe wenye kutimiza wajibu wao,” alionya.

Kamati hiyo ya siasa imeeleza kuridhishwa kwao na utekelezaji wa miradi hiyo, ikisema ni matokeo ya juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara,  Queen Sendiga, amepokea maagizo yaliyotolewa na Kamati hiyo, na akaahidi kusimamia kwa karibu kukamilika kwa miradi hiyo ifikapo Juni 30 mwaka huu.

Miongoni mwa miradi iliyowavutia wajumbe wa kamati hiyo ni ujenzi wa shule ya sekondari ya ufundi katika kata ya Bashay, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, ambayo iko katika hatua za mwisho kukamilika.

Wajumbe wamepongeza serikali kwa hatua hiyo, wakisema shule hiyo itawasaidia wanafunzi kuhitimu na kujiajiri, hivyo kupunguza utegemezi katika familia na kwa serikali.

Wananchi wa Mbulu nao wamemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwaletea maendeleo kupitia miradi hiyo, wakisema kuwa wanahisi kuguswa moja kwa moja na juhudi za serikali yao.

Hapa chini ni Picha mbalimbali wakati wa ziara hiyo wilayani Mbulu.

Picha zote na John Walter Muungwana blog.




















Post a Comment

0 Comments