Na John Walter -Babati
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga, amezindua rasmi huduma ya kusafisha damu (Dialysis) pamoja na huduma ya kipimo cha mfumo wa chakula katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, hatua inayolenga kupunguza gharama na usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Sendiga alisema kuwa mpango huu ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya na kuzisogeza karibu na wananchi.
"Huduma hii ni ya kisasa na muhimu sana kwa wakati huu, hasa ikizingatiwa kuwa magonjwa ya figo yanaongezeka kwa kasi duniani," alisema Sendiga.
Awali, wagonjwa waliokuwa wakihitaji huduma za kusafisha damu walilazimika kwenda Hospitali ya Rufaa ya Haydom au hospitali nyingine zilizoko mbali, jambo lililoongeza gharama na usumbufu mkubwa kwao na familia zao.
Kwa sasa, huduma hiyo inapatikana mkoani Manyara, na hivyo kuondoa adha ya safari ndefu.
Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Dkt. Yesige Mutajwaa, hospitali imeshatoa jumla ya rufaa 22 kwa wagonjwa waliokuwa wakihitaji huduma ya Dialysis kuanzia Julai 2024 hadi sasa.


Amesema baadhi ya wagonjwa walilazimika kuhamia kabisa mikoa yenye huduma hiyo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kugharamia safari mbili hadi tatu kwa wiki.
Mradi huo mkubwa umegharimu kiasi cha Shilingi milioni 522.5, ambazo zilitumika kununua mashine sita za kusafisha damu, mashine ya kupima mfumo wa chakula, na kufanya ukarabati wa jengo litakalotumika kutoa huduma hizo.
Aidha, kiasi cha Shilingi milioni 29.8 zilitumika kwa ajili ya mafunzo kwa watumishi wanaotoa huduma hizo maalum.
Dkt. Mutajwaa alisisitiza kuwa vifaa hivyo vya kisasa vitunzwe ipasavyo ili huduma iwe endelevu na wananchi waendelee kupata huduma bora kama ilivyokusudiwa na Serikali.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha huduma hizi muhimu kuwafikia wananchi wa Manyara,” aliongeza.
Huduma hii mpya ni mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Manyara na mikoa jirani, kwani sasa wanaweza kupata matibabu ya uhakika bila usumbufu wa safari ndefu na gharama kubwa.
0 Comments