F Huu hapa muonekano mpya wa chumba cha upasuaji watoto Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya baada ya maboresho makubwa | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Huu hapa muonekano mpya wa chumba cha upasuaji watoto Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya baada ya maboresho makubwa



Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya imefungua huduma za chumba cha upasuaji wa watoto (Pediatric Operating Theatre) baada ya kufanyiwa maboresho makubwa na kuwekewa vifaa tiba vya kisasa.

Maboresho hayo yamefanyika kwa ushirikiano wa Shirika la Kimataifa la Smile Train kutoka Marakani linaloratibu matibabu ya Mdomo wazi na shirika la Kids Operating Room (KidsOR) kutoka nchini Scotland linalojitolea kuboresha huduma za afya ya watoto kupitia uwekezaji kwenye miundombinu ya upasuaji.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo,Kaimu Mkurugenzi Dkt.Uwesu Mchepange amewashukuru wafadhili kwa msaada wao na kubainisha kuwa maboresho hayo yataongeza ufanisi wa utoaji huduma za upasuaji kwa Watoto ambapo pia yameunda mazingira rafiki na ya kuvutia kwa watoto wanaopata huduma za upasuaji yatakayosaidia kupunguza hofu kabla na baada ya upasuaji.

"Serikali kwa kushirikiana na wadau wamefanya maboresho haya makubwa kwenye vyumba vya upasuaji kwa ajili ya huduma za watoto,vyumba hivi sasa ni rafiki kwa ajili ya kutoa huduma kwa maana mazingira yake kuwa rafiki lakini kuwekewa vifaa vya kisasa kabisa"amesema Dkt.Uwesu 

Dkt.Mchepange pia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa nafasi kwa wadau wa maendeleo kushirikiana na serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini. 

Kwa upande wake,Veronica Kimwela, Msimamizi wa Miradi ya  Smile Train Tanzania na Jenn Perkison Mratibu wa KidsOR, ameshukuru hospitali kwa kutoa nafasi ya kushirikiana nao katika mradi huo muhimu na kuahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na hospitali hiyo pamoja na taasisi nyingine za afya nchini kwa manufaa ya watoto wa Tanzania.

"Kwa muda mrefu sana tumekuwa tukishirikiana na hospitali ya rufaa ya kanda ya Mbeya na kutokana na mahusiano mazuri tuliyokuwa nayo tumeweza kuwaletea chumba cha upasuaji cha watoto wadogo na tunaamini chumba hiki kitaleta mabadiriko kwa watoto wote watakaokuja kutibiwa"amesema   Veronica

Ufunguzi wa chumba cha upasuaji wa watoto kilichofanyiwa maboresho unatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kutoa huduma bora za upasuaji kwa watoto kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine ya jirani na kufanya hospitali hiyo kupiga hatua kubwa katika kuboresha afya ya watoto nchini Tanzania.









Post a Comment

0 Comments