F Jamii yatakiwa kuwa na Hofu ya Mungu na kukemea ukatili. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Jamii yatakiwa kuwa na Hofu ya Mungu na kukemea ukatili.


Na John Walter -Babati 

Siku chache baada ya tukio la kusikitisha la kubakwa na kuuawa kwa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Ayatsea, uongozi wa  SMAUJATA Wilaya ya Babati umetembelea kijiji cha Ayatsea kutoa elimu na kukemea vikali vitendo vya ukatili vinavyoendelea kushamiri kwa kufichwa ndani ya jamii.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Babati, Ezekiel Tlanka, ambaye pia ni Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Kaskazini, matukio zaidi ya manne ya ukatili yameripotiwa kutokea kijijini humo, lakini mara nyingi yamekuwa yakimalizwa kifamilia, jambo linalozidi kushusha utu na haki za waathirika.

“Vitendo hivi vinatia aibu na havifai kufumbiwa macho,  tunatoa rai kwa jamii kuwa na hofu ya Mungu na kusimama kidete kukemea na kuwafichua wanaojihusisha na tabia hizi chafu,” alisema Tlanka wakati wa ziara hiyo.

Katika hatua ya kushangaza, Tlanka alivamia mkutano wa kina mama uliokuwa ukilenga kufanya usuluhishi wa mgogoro baada ya kijana mmoja kumtukana mama yake kwa matusi makali.

Alilitumia tukio hilo kama mfano wa namna jamii inavyojaribu kumaliza mambo kimyakimya badala ya kufuata taratibu zinazostahili.

Kwa lengo la kusaidia waathirika na wanaohitaji msaada, alitoa namba yake ya mawasiliano pamoja na ile ya msaada wa bure ya serikali (116), na namba ya meseji (0765345777) kwa yeyote mwenye taarifa au anayehitaji msaada.

Aidha, timu ya SMAUJATA ilitembelea Shule ya Msingi Ayatsea na Sekondari ya Ayatsea ambapo walitoa elimu juu ya kupinga ukatili wa kijinsia, haki za watoto, na umuhimu wa kuripoti matukio yote ya ukatili kwa mamlaka husika.

Tukio hili limeibua mjadala mpana kuhusu usiri wa familia katika kushughulikia ukatili, na kuonesha haja ya haraka kwa jamii kushirikiana na vyombo vya dola ili kumaliza kabisa vitendo hivi ambavyo vinakatisha ndoto za watoto na kuvuruga misingi ya maadili.

Post a Comment

0 Comments