Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Njombe imetaka viongozi waliopo madarakani kuonyesha nini kimefanyika kwa kuwa Jumuiya hiyo inahitaji uwajibikaji na kufanya kazi ili kupeleka maendeleo kwa wananchi.
Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Njombe Dkt.Scholastika Kevela amebainisha hayo wilayani Ludewa wakati kamati ya siasa ilipofika wilayani humo kwa ziara ya kawaida yenye lengo la kujenga Chama na Jumuiya pamoja na kukumbushana mambo mbalimbali kuelekea kwenye uchaguzi.
"Kiongozi yeyote uliopo madarakani lazima utuonyeshe umefanya nini kwa hiyo hatuko tayari kuwa na viongozi wasio fanya kazi lakini nawashukuru viongozi wangu wa mkoa wa Njombe wakiwemo madiwani na wabunge kwa kuwa wanafanya kazi vizuri na sasa tunatoa hamasa wanaokuja wafanye kazi kwa mifanona kuacha alama"amesema Dkt.Scholastika Kevela
Kwa upande wake Anna Mwalongo ambaye ni mjumbe wa baraza UWT Taifa (Mbalaza) Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amekwisha acha alama hivyo ni wajibu kwa wanawake kwenda kuzisemea kazi zake kwa wananchi na kumtafutia kura aweze kupata ushindi mkubwa.
"Kiongozi wa UWT ukiona kuna changamoto kwenye eneo lako lazima utoe taarifa kwenye ngazi yako ya kata,wilayani ili ziweze kufanyiwa kazi hatutakiwi kukaa kimya kwasababu Rais Samia amefanya kazi kubwa na nzuri"Amesema Anna Mwalongo
Aziza Kiduda ni katibu wa UWT mkoa wa Njombe amesema ni wajibu wa viongozi wa UWT kwenda kuhamasisha wanawake kwenda kupiga kura kwa kuwa lengo ni kupata ushindi mkubwa.
"Ushindi wetu tunataka uwe wa kishindo utakaotikisa kwa kuwa sisi wanawake kwa idadi tuko wengi kwa hiyo tunatakiwa kuwa mbele kwenda kupiga kura"amesema Aziza
Nao baadhi ya wajumbe wa baraza la UWT wilaya ya Ludewa waliohudhuria kikao hicho akiwemo Agatha Kayombo wameshukuru uongozi ngazi ya mkoa kwa kufika wilayani humo na kutoa maelekezo ambapo wameahidi kwenda kufanyia kazi maelekezo ili Chama kiendelee kushika dola.
0 Comments