Na John Walter -Hanang'
Kijiji cha Dumbeta kilichopo Wilaya ya Hanang', mkoani Manyara sasa kimeunganishwa kikamilifu kwenye huduma ya umeme, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya wakazi wake.
Haya yamebainika wakati Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mkoa wa Manyara ilipotembelea mradi wa usambazaji umeme katika kijiji hicho.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Peter Toima, aliwataka wananchi wa Dumbeta kuchangamkia fursa hiyo kwa kuvuta umeme majumbani mwao ili waweze kunufaika na huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Natoa wito kwa viongozi wa kijiji wakiwemo Diwani, Mwenyekiti na Mtendaji kuhakikisha wanawahamasisha wananchi kuvuta umeme, tuhakikishe kila mwananchi anapata nishati hii kwa matumizi mbalimbali kama vile uboreshaji wa shughuli za biashara, elimu, afya na maisha ya kila siku,” alisema Mheshimiwa Toima.
Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Hanang’, Mhandisi Nadhir Yusufu, aliieleza Kamati hiyo kuwa hadi sasa jumla ya wananchi 27 tayari wameunganishwa na huduma ya umeme kati ya wananchi 89 waliokuwa bado hawajaunganishwa.
"Tunaendelea kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuunganishwa na umeme, tumejipanga kuhakikisha kila mwananchi katika kijiji hiki anapata huduma hii kwa wakati," aliongeza Mhandisi Nadhir.
Wananchi wa Dumbeta wamepokea kwa furaha hatua hiyo ya maendeleo, wakieleza kuwa uwepo wa umeme utachochea ukuaji wa uchumi wa kaya, kuongeza fursa za ajira kupitia shughuli za kiuchumi, pamoja na kuboresha huduma za kijamii.
Mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali kupitia TANESCO na Mpango wa REA kuhakikisha vijiji vyote nchini vinafikishiwa huduma ya umeme kwa maendeleo jumuishi ya Taifa.
0 Comments