F RC Manyara aboresha taarifa za mpiga Kura Babati. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

RC Manyara aboresha taarifa za mpiga Kura Babati.


Na John Walter -Babati, Manyara 

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, leo Mei 22, 2025, ameboresha taarifa zake za mpiga kura katika mtaa wa Babati, kata ya Babati, na kusisitiza umuhimu wa kila raia mwenye sifa kuhakikisha anashiriki katika zoezi hilo ili kupata haki ya kupiga kura ifikapo Oktoba mwaka huu.

Zoezi la uboreshaji wa taarifa za mpiga kura awamu ya pili lilianza Mei 16, 2025 na linahitimishwa rasmi leo Mei 22, 2025.

Sendiga aliwasili kituoni saa 4 asubuhi na kuelekea moja kwa moja katika kituo cha kujiandikisha, ambapo alitumia takribani dakika tano kukamilisha taratibu hizo. Baada ya kukamilisha uboreshaji wa taarifa zake, alipata fursa ya kuzungumza na wananchi waliojitokeza katika kituo hicho.

Katika hotuba yake, Sendiga aliwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuboresha taarifa zao na kujihakikishia ushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.

“Nimeona nijiunge nanyi… kama mnavyojua mimi ni mkazi wa Babati Mjini. Huko nyuma nimepiga kura sehemu nyingi. Nimekuja kurekebisha taarifa zangu; huko nyuma nilikuwa nikijiandikisha na kupiga kura maeneo mengine. Panapo majaliwa, mwaka huu nitapiga kura katika wilaya ya Babati mkoani Manyara,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Ushiriki wa viongozi katika zoezi hili ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha wananchi kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa kujisajili na kuboresha taarifa zao za mpiga kura.

Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Babati Mjini Edna Moshi amesema zoezi linaendelea vizuri katika Vituo vyote na ameongeza kuwa Wananchi takribani 1294 wamejiandikisha, Wananchi 1599 wameboresha taarifa na Wananchi 498 wamefuta taarifa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Awamu ya Pili.

Picha mbalimbali wakati wa zoezi hilo.






Post a Comment

0 Comments