Na John Walter -Simanjiro
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Peter Toima, ametoa onyo kali kwa baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM wilayani Simanjiro wanaokiuka taratibu za chama kwa maslahi binafsi, akisisitiza kuwa chama hakiwezi kuvumilia vitendo vya kiholela vinavyokiuka maadili ya chama.
Toima ametoa kauli hiyo akiwa katika ziara ya kichama wilayani humo, akiwa ameambatana na Kamati ya Siasa ya Mkoa, ambapo walikutana na viongozi pamoja na wanachama wa CCM katika kikao kilichofanyika katika Kijiji cha Narakauo, Kata ya Loiborsiret, kikihusisha Tarafa za Terrati na Emboret.
Katika kikao hicho cha ndani, baadhi ya wajumbe walilalamika kuhusu tabia ya baadhi ya viongozi kupachika majina ya wagombea kiholela na kuanza kampeni za wazi kwa watu wanaowapendelea kushika nafasi za ubunge na udiwani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Malalamiko mengine ni kuhusiana na uchaguzi usio halali wa wasaidizi wa mabalozi katika baadhi ya mashina, licha ya uchaguzi huo kukamilika rasmi mwaka 2022 kulingana na taratibu za chama.
Toima amewasikiliza kwa makini wanachama na viongozi waliotoa kero zao, na kutoa majibu ya moja kwa moja, akiahidi kuwa chama kitachukua hatua stahiki dhidi ya wanaokiuka taratibu.
Amesisitiza kuwa nidhamu ya chama ni nguzo ya mshikamano na mafanikio ya CCM.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer, amefunguka kwa kusema kuwa wapo watu wachache ndani ya chama wanaojifanya “kila kitu” na wanaharibu chama kwa maslahi yao binafsi.


“Wale wanaojifanya ni kila kitu watachukuliwa hatua kali na chama hakitawavumilia. Utaratibu lazima ufuatwe,” alisema Laizer.
Laizer pia alimshukuru Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Peter Toima, pamoja na Kamati ya Siasa ya Mkoa kwa kufika Simanjiro na kukemea vitendo visivyokuwa vya kiungwana na vinavyoonyesha kutokuwepo kwa mapenzi ya kweli kwa chama.
Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Shabani Mrisho Lula, ameleza kuwa chama kimepokea rasmi malalamiko yote kutoka kwa wanachama na kimepanga kukutana na viongozi wa chama wilaya ya Simanjiro kuanzia tarehe 13 hadi 15 Mei 2025.


Amesema anaamini changamoto hizo zitatatuliwa kwa pamoja na uchaguzi mkuu utafanyika kwa amani na kwa kuzingatia taratibu zote za chama.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, pamoja na viongozi wengine walioshiriki kikao hicho, walimsifu Toima kwa kuwaongoza kwa uwazi na kwa juhudi zake za kujenga mshikamano ndani ya chama wilayani humo.
0 Comments