Na John Walter -Simanjiro.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Peter Toima, amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Simanjiro, Tarafa ya Mirerani, ambapo aliwahimiza wanachama wa chama hicho kuwa na mshikamano, kushirikiana katika ujenzi wa Chama na kudumisha uhai wake kwa vitendo.
Katika ziara hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama ngazi za wilaya, kata, matawi na mashina, Mheshimiwa Toima aliwataka wanachama kuendeleza mapenzi kwa Chama badala ya kuendekeza makundi na ushabiki usio na tija.
"Chama kipo kwa ajili ya kila mmoja wetu, na ni wajibu wetu kukilinda na kukitumikia kwa moyo wa uzalendo," alisema Toima.
Akiwa katika kata ya Endiamtu, alihimiza umuhimu wa kuendelea kuchangia ujenzi wa ofisi ya CCM ya kata hiyo kama ishara ya kujenga Chama imara chenye misingi ya maendeleo.
Aidha, alisisitiza kuwa kwa mafanikio ya Chama kuonekana, ni lazima wanachama walipe ada za uanachama, wafanye mikutano ya kikanuni na kuachana kabisa na migogoro ya ndani.
Kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Mwenyekiti Toima alieleza kuwa ana imani kuwa CCM itashinda kwa asilimia mia moja, kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Hata hivyo, alieleza wasiwasi wake juu ya baadhi ya maeneo ya Simanjiro ambapo uchaguzi wa mashina umefanyika kinyume na utaratibu, akisisitiza kuwa uchaguzi wa Chama ulimalizika rasmi mwaka 2022, na hakuna nafasi mpya wala wasaidizi wa mabalozi.
“Waliofanya uchaguzi wamepoteza muda wao, waache makundi na waendelee na shughuli nyingine,” alisema.
Toima alikemea vikali tabia ya baadhi ya watu kuwania nafasi za udiwani na ubunge kwa tamaa binafsi, akitoa mfano wa uchaguzi wa mwaka 2020 ambapo kulikuwa na wagombea 20 wa ubunge katika Wilaya ya Simanjiro.
Alisisitiza kuwa nafasi hizo ni chache na si lazima kila mtu awe mbunge au diwani. "Wengine fanyeni kazi zingine za Chama au jamii, si lazima wote tuwe viongozi wa kuchaguliwa," aliongeza.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Ndg. Shabani Mrisho, aliwahimiza wanachama kuwa wamoja na kuachana na makundi yanayodhoofisha Chama.


Alisisitiza kuwa mafanikio ya CCM yanategemea mshikamano wa kweli na utii kwa taratibu na kanuni za Chama.
Ziara hiyo imeacha gumzo la matumaini miongoni mwa wanachama wa CCM wilayani Simanjiro, huku ikionekana kuwa chachu ya kuimarisha misingi ya uongozi bora, mshikamano na maendeleo ya Chama kuelekea uchaguzi mkuu ujao Oktoba mwaka huu.
Picha mbalimbali katika ziara wilayani Simanjiro.
0 Comments