Na John Walter -Simanjiro, Manyara
Wanafunzi zaidi ya 17,000 wamesoma kupitia juhudi za Eclat Development Foundation, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utoaji wa elimu kwa watoto na vijana kutoka familia duni, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Peter Toima, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Manyara waliotembelea ofisi za Eclat Development Foundation zilizopo Emboret, Wilaya ya Simanjiro, Toima alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora bila kujali changamoto za kiuchumi zinazowakabili.


"Mpaka sasa, zaidi ya wanafunzi 17,000 wamesoma kupitia mipango mbalimbali ya Eclat, ikiwa ni pamoja na ufadhili wa ada, vifaa vya shule, na ujenzi wa miundombinu ya elimu," alisema Toima. "Tunafanya kazi kwa kushirikiana na jamii na wadau mbalimbali kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kusoma."
Wajumbe wa Kamati ya Siasa walionesha kuridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na taasisi hiyo, wakiahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo zinazochangia maendeleo ya elimu na ustawi wa jamii mkoani Manyara.
Taasisi ya Eclat Development Foundation imejipatia sifa kwa namna inavyobadilisha maisha ya vijana kupitia elimu, ikisisitiza uwajibikaji, ushirikiano na kujitolea kama nguzo za mafanikio yake.



