Na John Walter -Babati
Zaidi ya matukio 2,000 ya ukatili yameripotiwa katika Mkoa wa Manyara ndani ya kipindi cha miezi minne pekee, hali inayoashiria ongezeko kubwa la vitendo hivyo vinavyotishia ustawi wa jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amefichua takwimu hizo leo alipokuwa akiongoza kikao maalumu kilichowakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali, wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Kamati za Usalama, Wakurugenzi, Makatibu Tawala pamoja na wadau wa maendeleo kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kukabiliana na ukatili huo.
Kwa mujibu wa RC Sendiga, kutoka Januari hadi Mei 2025, jumla ya matukio 2,201 ya ukatili yameripotiwa katika mkoa mzima. Wilaya ya Hanang imeongoza kwa kuwa na matukio 668, ikifuatiwa na wilaya nyingine kwa idadi tofauti.
“Kasi ya kuongezeka kwa ukatili ni ya kutisha, tunahitaji kuchukua hatua za haraka, za pamoja na madhubuti kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya vitendo hivi,” amesema RC Sendiga.
Aidha, ametoa wito kwa watumishi wa umma na taasisi zinazohusika kushughulikia matukio ya ukatili kutimiza wajibu wao kwa weledi na uadilifu, akisisitiza kuwa baadhi ya watendaji wamekuwa wakihujumu mchakato wa haki kwa kupokea hongo au kushindwa kushughulikia kesi kikamilifu.
“Kesi za ukatili zimekuwa ni chanzo cha watu wachache kujipatia fedha. Hii ni aibu kubwa. Lazima tuikomeshe,” amesisitiza.
Hata hivyo wadau mbalimbali wakiwemo wanaharakati kutoka Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA), wakishirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, wameendelea kutoa elimu kwa jamii kuepuka vitendo hivyo licha ya changamoto wanazokumbana nazo, hasa ukosefu wa fedha na usafiri, hali inayokwamisha juhudi zao za kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga ameahidi kuendeleza mashirikiano na wadau wote, pamoja na kuhakikisha rasilimali muhimu zinapatikana ili kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili mkoani Manyara.
0 Comments