Ikiwa rasmi Chuo kikuu Cha Dodoma tawi la Njombe kimesaini mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho katika mtaa wa Kihesa uliopo halmshauri ya mji wa Njombe baina ya chuo hicho na Kampuni inayokwenda kutekeleza mradi huo ya Dimetoclasa Real hope Limited.
Hatimaye uongozi wa kata ya Utalingolo kwa kushirikiana na wataalamu wa Idara ya ardhi Halmashauri ya Mji Njombe nao pia wamekamilisha zoezi la uwekaji wa alama za mipaka (Bikon) kwenye ardhi yenye ukubwa wa takribani ekari 300 kata ya Utalingolo katika kijiji cha Ihalula kwa chuo kikuu Cha Dodoma tawi la Njombe kwa ajili ya mazoezi ya vitendo.
Akiongoza zoezi la uwekaji wa alama za mipaka Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe ambaye pia ni diwani wa kata ya Utalingolo Erasto Mpete amewataka wananchi wa kijiji hicho kuendelea kuimarisha ulinzi wa eneo hilo kwa maslahi ya watanzania.
"Niwaombe wananchi waendelee kulinda hili eneo kwa maslahi ya kizazi chetu na vizazi vijavyo,lakini pia wananchi muwe na subra kwasababu ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya Chuo hiki unaenda kwa awamu na kwa hatua ya kwanza ujenzi umeanza ofisi kuu pale Njombe mjini na huku ni eneo la mazoezi kwa vitendo kwa hiyo wananchi wanaozunguka hili eneo huko mbeleni watanufaika kiuchumi" amesema Mpete
Mpete ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha za ujenzi wa Chuo kikuu Njombe ambapo pia ametoa pongezi kwa mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka, Mbunge wa Njombe mjini Deodatus Mwanyika pamoja na Chama cha Mapinduzi kwa kuendelea kushikamana ili kukuza uchumi na miradi ya maendeleo mkoani Njombe.
Baadhi ya wakazi wa Utalingolo akiwemo Ben Mlyonga pamoja na Stanley Nyangachi wameshukuru serikali kwa kukubali kujenga Chuo kikuu mkoa wa Njombe kwa kuwa nao pia wanakwenda kunufaika na uwepo wa Chuo kikuu.
"Kimsingi hata sisi wananchi wa Utalingolo tunakwenda kunufaika na Chuo hiki lakini na sisi tunawakaribisha wawekezaji kwasababu fursa zitafunguliwa kwenye maeneo yetu "amesema Nyangachi
Kwa mujibu wa Naibu mratibu wa mradi wa HEET toka Chuo kikuu cha Dodoma Dkt.Happiness Nnko alipozungumza mkoani Njombe wakati wa kusaini mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho alisema kiasi cha shilingi Bilioni 17.17 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu sita ya msingi katika chuo hicho inayoanza kujengwa katika mtaa wa Kihesa mjini Njombe.
Aidha Mwenyekiti wa Baraza la Chuo kikuu Cha Dodoma Profesa Rwekaza Mukandala alisema kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi kwenye vyuo vikuu Nchini Rais Samia aliamua kuongezwa kwa matawi ya vyuo Likiwemo tawi la Njombe.
Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka alisema suala la Elimu kwa wakazi wa Njombe ni muhimu na wanahamasa kubwa ya kusomesha watoto wao.
Naye mkurugenzi wa kampuni inayokwenda kutekeleza mradi huo ya Dimetoclasa Real hope Limited Bwana Dickson Mwipopo aliahidi kufikisha mitambo eneo la ujenzi katika mtaa wa Kihesa ndani ya wiki hii na kuanza kazi mara Moja.
Chuo kikuu hicho hadi kukamilika kwake kitatumia shilingi bilioni 20.
0 Comments