Serikali imeombwa kuzipunguzia kodi hospitali zinazo milikiwa na taasisi za dini ili kurahisisha uendeshaji kwa kuwa hazijaanzishwa kwa lengo la kufanya biashara zaidi ya kutoa huduma kwa wananchi kutimiza takwa la kanisa kutoa huduma ya kimwili na kiroho.
Wito huo umetolewa na Pandre Inocent Chaula ambaye ni katibu wa afya na katibu wa Mhashamu Askofu Ausebius Kyando Jimbo Katoliki la Njombe wakati wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Ukristo 2025 iliyofanyika katika hospitali ya St.Joseph Ikelu iliyopo halmashauri ya mji wa Makambako.
"Hospitali imeletwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na sio biashara tuombe tusaidiane katika huduma hizi,tunapata changamoto ya katika uendeshaji michango mingi,kodi nyingi sasa tuwaombe viongozi wa serikali mliopo mtusemee kama kituo cha huduma na sio biashara"amesema Padre Chaula
Amesema "Kanisa linamuhudumia mtu kimwili na kiroho kwa miaka hii ya karibuni sisi sekta binafsi hasa za makanisa tunaonja ukali huo hivyo basi tuiombe serikali iwe inatufikiria katika jambo hilo na pia ugumu katika mambo ya bima kwasababu vifurushi vya bima vilivyoletwa kidogo vinakandamiza mtoa huduma"
Amewataka wahudumu wa afya kuwa chachu ya matumaini kwa wagonjwa ambapo pia amepongeza hospitali kwa kutoa huduma za uchunguzi wa afya bure kwa wananchi 412 huduma iliyotolewa siku mbili hospitalini hapo.
Awali akisoma taarifa ya wafanyakazi wa hospitali hiyo Dkt.Policap Nyengela amesema licha kazi kubwa ya utoaji wa huduma inayofanywa ikiwemo za kibingwa lakini wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa vipimo vikubwa hususani MRI vipimo ambavyo vingeweza kusaidia kupunguza safari za kusafirisha wagonjwa sehemu nyingine kufuata kipimo hicho.
Nao baadhi ya wananchi akiwemo Hanipher Malekela na Osmond Mkungilwa waliofika kwa ajili ya kufuata huduma katika hospitali hiyo wameshukuru kwa huduma zinazotolewa huku wakiomba watumishi kuto vunjika moyo kwenye utumishi wao.
"Kazi hii ni wito kwa hiyo wawe na moyo huo wa kujitolea wala wasivunjike mioyo kutokana na Changamoto hasa za wagonjwa kwa kuwa mgonjwa anafika hospitali akiwa na matarajio yake"
Kwa mujibu wa katibu wa afya na katibu wa Mhashamu Askofu Ausebius Kyando amesema kuwa Askofu amepokea changamoto na yuko tayari kushughulikia zilizopo katika mamlaka yake na kwenda kuzisemea nyingine katika mamlaka za ngazi ya juu.
0 Comments