F Wananchi wa Hidet wamshukuru Dkt Samia kwa mradi wa maji wa Bilioni 1.5 | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wananchi wa Hidet wamshukuru Dkt Samia kwa mradi wa maji wa Bilioni 1.5



Na John Walter -Hanang', Manyara 

Wananchi wa Kata ya Hidet, Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara wamefurika kwa shangwe na furaha kushuhudia utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa na Wakala wa Maji Vijijini na Mijini (RUWASA) kutoka Ziwa Bassotuang’, mradi unaogharimu Shilingi bilioni 1.5.

Katika tukio la ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Manyara, wananchi walijitokeza na bango kubwa lililosomeka: “Tunamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi wa maji wa Shilingi Bilioni 1.5 kwa Kata ya Hidet. Mama Hana Deni na Wana Hidet, Tutamlipa Oktoba 2025.”

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Peter Toima, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Bassotughang’, alisema mradi huo mkubwa ni uthibitisho wa utekelezaji wa ilani ya CCM na dhamira ya dhati ya serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuboresha maisha ya wananchi.

“Serikali ya Rais Samia inatenda, Mradi huu ni wa kimkakati, na tunahitaji wananchi na viongozi kushirikiana kulinda chanzo hiki cha maji, Ziwa Bassotuang’ ni zawadi kutoka kwa Mungu; tusikubali shughuli za kibinadamu kuliharibu,” alisema Toima huku akiipongeza RUWASA kwa utekelezaji bora wa mradi huo.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, ambaye pia ni msimamizi mkuu wa shughuli za serikali mkoani humo, ameeleza kuwa serikali itasimamia kikamilifu utunzaji wa ziwa hilo, akionya kuwa eneo hilo lina kina kirefu na si salama kwa shughuli za kawaida za binadamu.

"Hatutaruhusu shughuli za kibinadamu karibu na ziwa, lengo ni kuhakikisha maji haya yanabaki salama na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo," aliongeza Sendiga.

Kwa mujibu wa Mhandisi wa RUWASA, Felix Mollel, mradi huo umehusisha ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 200,000, mtandao wa bomba wa kilomita 29 ambao tayari umekamilika kwa kiasi kikubwa, pamoja na vituo vya kuchotea maji 26, ambapo vituo 21 tayari vimekamilika na 18 kati ya hivyo vikiwa vinatoa huduma.

“Mradi huu utahudumia zaidi ya wananchi 4,600 kutoka Kata ya Hidet na vijiji jirani, tunatarajia kuukamilisha ifikapo mwezi Agosti mwaka huu,” alisema Mhandisi Mollel.

Serikali imesisitiza kuwa iko tayari kuendelea kutoa huduma kwa wananchi muda wote, huku ikiendelea kutekeleza ilani ya CCM inayotaka kila mwananchi kupata huduma ya maji safi na salama kwa umbali usiozidi mita 400 kutoka nyumbani kwake — ili kuwaondolea adha ya kutembea mbali na kuwapa nafasi ya kushiriki shughuli za maendeleo.

Post a Comment

0 Comments