Na John Walter- Babati
Diwani wa Kata ya Ufana, Mheshimiwa Bernard Bajuta amepongezwa kwa utekelezaji madhubuti wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha miaka mitano, ambapo miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa na kuboresha maisha ya wananchi wa kata hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla iliyofanyika katika shule ya sekondari Ndeki, Mheshimiwa Bajuta alieleza mafanikio yaliyopatikana, likiwemo suala la mawasiliano ya simu ambayo sasa yanapatikana tofauti na miaka ya nyuma ambapo kata hiyo haikuwa na huduma hizo muhimu.
Alisema hali hiyo imerahisisha mawasiliano kati ya wananchi na taasisi mbalimbali, hivyo kuchochea maendeleo.
Katika jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi, Bajuta alisema kuwa vikundi 15 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vimenufaika na mikopo ya Halmashauri ambapo jumla ya shilingi milioni 67.5 zimetolewa kwa ajili ya shughuli za kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wa huduma za maji, Diwani huyo alisema mabomba chakavu yameanza kuondolewa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika.
Alisema kuwa serikali imetenga shilingi milioni 18 kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Guse–Ufana, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri na usafirishaji wa mazao ya kilimo.
Akizungumzia suala la umeme, Bajuta alisema kuwa kila kijiji katika kata ya Ufana sasa kinapata huduma hiyo muhimu, huku vitongoji sita kati ya kumi vikitarajiwa kuunganishwa na umeme muda wowote kuanzia sasa.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Mhe. John Noya, alisema kuwa mradi wa maji wa Madunga umefikia asilimia 90 ya ukamilishaji, na unatarajiwa kuhudumia wananchi wa tarafa ya Bashnet yenye kata sita za Nar, Ufana, Bashnet, Secheda, Madunga na Qameyu.
Madiwani wa kata za Secheda, Nar, Ufana na Madunga walimpongeza Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo, wakisema kuwa kutokana na jitihada kubwa alizofanya katika kata zao, ataibuka mshindi kwa kura nyingi katika uchaguzi ujao.
Diwani Bajuta aliongeza kuwa shilingi bilioni 1.4 zimetolewa na serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo, ikiwa ni matokeo ya ushawishi mkubwa alioufanya kwa niaba ya wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Dinamu, Joseph Mandoo, alieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika Jimbo la Babati Vijijini ni ushahidi kuwa Mbunge Sillo ni kiongozi makini, na wananchi hawapaswi kumkosa tena kwenye uchaguzi ujao.
Bajuta ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake mahiri uliopelekea mafanikio makubwa katika kata ya Ufana.
Pia alimpongeza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, kwa sapoti yake ya karibu katika kuhakikisha maendeleo yanatimia.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Madiwani wa Viti Maalum wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, ambao walielezea kuridhishwa kwao na kasi ya maendeleo katika kata hiyo.
0 Comments