F Kijana afariki Dunia kwa Kushambuliwa na Kundi la Fisi Babati. | Muungwana BLOG

Kijana afariki Dunia kwa Kushambuliwa na Kundi la Fisi Babati.



Na John Walter -Babati

Kijana Freddy Peter, mwenye umri wa kati ya miaka 25 hadi 30, mkazi wa Kijiji cha Seloto wilaya ya Babati, amefariki dunia kwa majeraha mabaya baada ya kushambuliwa na kundi la fisi usiku wa kuamkia jana, wakati akirejea nyumbani kutoka kwenye msiba wa jirani.

Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea majira ya saa sita usiku, umbali mfupi kutoka makazi ya marehemu. 

Inadaiwa kuwa licha ya juhudi za wananchi waliokusanyika kwa wingi na kuwasha moto ili kuwatisha wanyama hao wakali, fisi hao waliendelea kuzagaa eneo hilo, jambo lililoibua hofu kubwa kwa wakazi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lotto,  Francis Leonce, ambaye alifika eneo la tukio, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema tayari wamewasiliana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) ili kuja kuwasaidia kuwaua fisi hao ambao wamesababisha taharuki kubwa kijijini.

“Tumetoa maagizo kwa walimu wakuu wa shule zote za msingi na sekondari ndani ya kijiji chetu kuzuia wanafunzi kuwahi sana asubuhi kwenda shuleni hadi hali itakapotulia. Usalama wa watoto wetu ni wa kwanza,” alisema Mwenyekiti Leonce.

Wananchi wa Seloto wamesema kwa sasa wanaishi kwa hofu kubwa kutokana na uwepo wa vichaka vikubwa na mashamba yaliyotapakaa mazao ambayo huwavutia fisi, na kufanya maeneo hayo kuwa hatarishi. Wanafunzi nao wameeleza wasiwasi wao wa kwenda shuleni hasa wakati wa asubuhi kabla ya jua kuchomoza.

Marehemu Freddy Peter ameacha mke na watoto wawili. 

Mabaki ya Mwili wake yamehifadhiwa katika hospitali ya Dareda Mission ambayo ipo karibu na kijiji hicho kusubiri taratibu za mazishi.

Tukio hili limezua hofu juu ya usalama wa binadamu katika maeneo hayo, huku wananchi wakitaka hatua za haraka kuchukuliwa dhidi ya wanyama wanaovamia makazi yao.

Post a Comment

0 Comments