F Mbunge wa Babati Mjini atoa Shukrani kwa Wananchi, asisitiza "Oktoba tunatiki' | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mbunge wa Babati Mjini atoa Shukrani kwa Wananchi, asisitiza "Oktoba tunatiki'



Na John Walter -Babati 

Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Mheshimiwa Paulina Gekul, amewashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa imani waliyoionesha kwake kwa kumchagua kuwa mwakilishi wao kwa kipindi cha miaka mitano.

Ametoa shukrani hizo wakati wa mkutano wa hadhara uliohitimisha ziara yake ya kutembelea kila mtaa na kijiji ndani ya jimbo hilo kwa lengo la kuwasikiliza wananchi na kupokea maoni yao.

Akizungumza katika mkutano huo, Mheshimiwa Gekul alisema:

“Hata nilipopita kwenye bonde la mauti kwa kusingiziwa, mlikuwa pamoja na mimi. Mlinipa moyo na kuniunga mkono. Leo narudi kwenu nikiwa na kichwa juu kwa sababu ya kazi tuliyoifanya kwa pamoja.”

Katika hotuba yake, Gekul alitaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano akiwa madarakani, akisisitiza kuwa maendeleo hayo yametokana na ushirikiano kati ya wananchi na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Gekul alieleza kwamba katika kipindi cha uongozi wake, Jimbo la Babati Mjini limepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali:

Elimu, Afya, Maji, Umeme na Kilimo: Ameeleza kuwa miradi mikubwa ya maendeleo imeboresha maisha ya wananchi.

Huduma za Afya: Zaidi ya magari ya wagonjwa 1,200 yamesambazwa nchi nzima, huku Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara iliyopo Babati Mjini ikipata mitambo ya kusafisha damu, hatua iliyopunguza gharama na usumbufu kwa wagonjwa.

Huduma za Dharura: Hospitali za wilaya zaidi ya 129 zimeboreshwa ili kutoa huduma za dharura kwa haraka.

Maji: Upatikanaji wa maji katika Jimbo la Babati Mjini umefikia asilimia 98.

TASAF: Imefikia kila kijiji na mtaa, ikiwasaidia wananchi maskini.

Ruzuku ya Mafuta: Serikali imeendelea kutoa ruzuku kwenye vituo vya mafuta ili bei zisipande kupita kiasi.

Miundombinu ya Usafiri: Treni ya mwendokasi imekuwa kielelezo cha maendeleo ya utawala wa Dkt. Samia.

Mradi wa Umeme wa Mwalimu Nyerere: Gekul amesema mradi huu wa trilioni saba umeondoa adha ya upungufu wa umeme hadi kwenye vitongoji.

Mbunge huyo pia ametangaza mpango wa kutenga bajeti kwa ajili ya kuondoa magugu maji katika Ziwa Babati, ili kuimarisha shughuli za uvuvi. 

Pia, amesema huduma za wakina mama wajawazito zimeboreshwa kwa kujengewa wodi maalum na majengo ya kufungulia.

Kwa upande wa michezo, Gekul amesema amenunua mipira na jezi kwa ajili ya kila mtaa na kijiji katika kata zote za Babati Mjini, ili kuendeleza vipaji vya vijana.

Akiwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, Gekul amesema:

"Oktoba tunatikisa na Rais, tutampa kura za kutosha. Kiongozi huyu amefanya makubwa na bado ana maono makubwa zaidi kwa taifa letu."

Amesema kuwa hajawahi kukaa kimya katika kutetea maslahi ya wananchi wa Babati Mjini, na kwamba amewatumikia kwa upendo, uwazi na uwajibikaji. 


  



Post a Comment

0 Comments