Na John Walter -Babati
Wakulima wa Wilaya ya Babati, hususan wa ukanda wa Mbugwe mkoani Manyara, wameonyesha mwitikio mkubwa katika kulima zao la karanga kufuatia utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo chake cha Naliendele.
Utafiti huo umebainisha kuwa mazingira ya eneo hilo yanafaa kwa kilimo cha karanga na kwamba zao hilo lina soko la uhakika, hatua ambayo imewapa matumaini wakulima na kuchochea hamasa ya kulima kwa tija.
Mtafiti kutoka TARI Naliendele, Bw. Anthony Bujiku, amesema Tanzania ipo katika nafasi nzuri kwenye uzalishaji wa karanga ukilinganisha na mataifa mengine ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ameeleza kuwa Tanzania ina takribani hekta milioni tatu zenye rutuba zinazofaa kwa kilimo cha karanga, lakini kwa sasa ni hekta milioni moja na nusu pekee ndizo zinazotumika.
“Tunayo ardhi ya kutosha na mbegu bora, hivyo tunawahimiza wakulima watumie mbegu zilizofanyiwa utafiti ili kuongeza tija,” amesema Bw. Bujiku.
Mkulima kutoka Kijiji cha Kiru, Jitu Vrajilal Son, ambaye shamba lake limehusika moja kwa moja kwenye utafiti wa mbegu bora za karanga, amesema kuwa TARI imekuwa mkombozi mkubwa kwao.
“Tulikuwa tukipanda kienyeji, lakini sasa tunatumia mbegu bora na teknolojia ya kisasa, matokeo ni mazuri na ya kutia moyo,” amesema kwa furaha.
Wakulima wengine waliopata nafasi ya kushiriki kwenye mafunzo na majaribio ya kilimo hicho wamesema utafiti uliofanywa na TARI umewapa matumaini makubwa na wameiomba Serikali kuendeleza utafiti kama huo kwenye mazao mengine pia, ili kuinua kilimo kwa ujumla.
Serikali kupitia wizara husika inaendelea kutuma wataalamu wake katika maeneo mbalimbali ili kufanya tafiti zaidi kuhusu zao hilo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji na kuhakikisha wakulima wanapata mazao yenye tija na soko la uhakika.
Kwa hatua hii, Babati inaelekea kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya uzalishaji wa karanga nchini, na mfano wa kuigwa kwa maeneo mengine ya Tanzania.
0 Comments