Na John Walter -Dodoma
Katika jitihada za kujenga jamii yenye usawa na haki kwa wote, mradi wa Tuinuke Pamoja unaotekelezwa na TGNP kwa kushirikiana na Aga Khan Foundation na kufadhiliwa na Ubalozi wa Ireland, umeendelea kuleta mwamko na majadiliano ya kina kupitia midahalo ya kijamii inayofanyika katika kata za Kidoka (Chemba), Keikei na Suruke (Kondoa).
Midahalo hii inalenga kuchambua kwa kina vikwazo vinavyozuia upatikanaji wa usawa wa kijinsia katika jamii na kutafuta suluhu endelevu kwa changamoto zinazojitokeza. Kwa kuzingatia umuhimu wa ushirikishwaji, midahalo inawahusisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa kijamii na wa dini, wazee wa mila, wazee maarufu, vikundi vya kijamii pamoja na watu wenye ulemavu.
Katika midahalo hiyo, washiriki wamekuwa wakieleza uzoefu wao kuhusu masuala ya kijinsia, mila na desturi zinazokwamisha maendeleo ya wanawake na wasichana, pamoja na mapendekezo ya jinsi jamii inaweza kuondokana na mifumo kandamizi. Kupitia mchakato huu shirikishi, jamii inahimizwa kufikiria upya mitazamo na mienendo inayozuia maendeleo jumuishi.
Mradi huu umeweka mkazo mkubwa katika kushirikisha sauti za watu walioko pembezoni mwa maendeleo, kwa kutambua kuwa hakuna usawa wa kijinsia unaoweza kufikiwa bila ushiriki wa makundi yote ya jamii.
Kwa pamoja, tunaamini kuwa "Tukiinuka pamoja, tunaweza kujenga jamii yenye usawa kwa wote."
0 Comments