Airtel Money Tanzania kwa kushirikiana na Mastercard, kupitia teknolojia ya Network International, inayofuraha kutangaza upya huduma yake ya kadi ya malipo ya kidijitali inayojulikana sasa kama Airtel Money Global Pay— ambayo ni suluhisho la malipo ya kidigitali lililo salama, rahisi na linaloendana na maisha ya kisasa.
Kadi hii ya kidijitali ya Airtel Money Global Pay inapatikana kupitia programu ya MyAirtel App. Kupitia huduma hii, Watanzania sasa wanaweza kulipia bidhaa au huduma kwenye majukwaa ya kimataifa kwa ajili ya manunuzi, masomo, safari, au burudani moja kwa moja kutoka kwenye simu zao za mkononi. Airtel Money Global Pay ni uvumbuzi wa kipekee unaodhihirisha dhamira ya Airtel katika kuendeleza urahisi wa kidijitali, usalama wa miamala na ujumuishaji wa kifedha kwa wote.
Akiongoza uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Money, Adolf Kasengenya, alieleza kuwa Airtel Money Global Pay ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya Serikali ya kuwezesha Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa kidijitali wa kimataifa kwa njia salama, ya kisasa, na isiyo na utegemezi mkubwa kwa pesa taslimu.
“Ushirikiano huu wa kuunganisha mtandao wa malipo wa Mastercard ndani ya mfumo wa Airtel Money ni hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu ya kifedha ya kidijitali hapa nchini. Airtel Money Global Pay inaendana moja kwa moja na vipaumbele vya Benki Kuu ya Tanzania kuhusu mifumo ya malipo, ujumuishaji wa kifedha, na kuondoa mipaka ya matumizi ya fedha. Huduma hii inaleta njia salama na rahisi kwa Watanzania—wenye akaunti za benki na wasio nazo—kushiriki katika uchumi wa kidijitali wa dunia,” alisisitiza.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla iliyofanyika Johari Rotana, Mkurugenzi wa Airtel Money, Bw. Andrew Rugamba, alieleza kuhusu umuhimu wa Airtel Money Global Pay katika kupanua wigo wa huduma za malipo ya kimataifa kwa wateja wa Airtel Tanzania.
“Tumewarahisishia wateja wetu kufanya malipo ya kimataifa kutoka hapa nchini bila kuhitaji akaunti ya benki. Pakua tu MyAirtel App, wasilisha maombi ya Global Pay, weka salio na anza kufanya manunuzi, kuangalia filamu au kulipia huduma zako kimataifa kwa urahisi na usalama,” alisema.
Rugamba aliongeza: “Airtel Money Global Pay si kadi tu ya kidijitali. Ni pasipoti yako kwenda kwenye dunia yenye ushindani wa kibiashara na burudani ya kimataifa, moja kwa moja kutoka kwenye simu yako ukiwa nyumbani. Tunawashukuru sana Mamlaka zinazohusika kwa kuunga mkono mageuzi haya ya mfumo wa malipo na pia washirika wetu kwenye teknolojia, Network International, kwa kuwezesha ufanisi wa huduma hii inayoiwezesha Airtel Money Global Pay kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.”
Kwa muda mrefu, Watanzania wanaonunua, kusoma, kucheza michezo ya kwenye simu au kufanya biashara mtandaoni wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali katika kufanya miamala ya kimataifa. Changamoto hizo ni pamoja na: Ukosefu wa kadi zinazokubalika kimataifa, kutokueleweka kwa viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni, gharama kubwa za uhamisho au malipo kupitia njia za kawaida, hofu ya usalama na utapeli, na kukataliwa kwa malipo ya mitandao ya simu na majukwaa ya kimataifa.
Kwa kuweka kadi ya kidijitali iliyounganishwa na Mastercard moja kwa moja ndani ya programu maarufu ya MyAirtel App, Airtel Money Global Pay inasaidia; kutolewa papo kwa papo; Kujaza salio kupitia Airtel Money kwa shilingi za kitanzania, viwango vya fedha za kigeni vinavyoonekana moja kwa moja, Udhibiti wa matumizi kwa wakati halisi, na Kukubalika kimataifa—bila haja ya kwenda benki au kuwa na kadi halisi
Ubadilishaji jina kutoka Airtel Mastercard kwenda Airtel Money Global Pay unakuja sambamba na maboresho mapya yanayolenga kuongeza usalama na uzoefu wa mtumiaji. Sasa ikiwa imeunganishwa kikamilifu ndani ya MyAirtel App, watumiaji wanaweza: kutoa na kujaza salio kwenye kadi papo hapo; kubadilisha mwonekano wa kadi; kuona viwango vya fedha kwa wakati halisi; kufuatilia au kusitisha miamala moja kwa moja kupitia simu yao; na maboresho haya yanarahisisha zaidi matumizi ya malipo ya kimataifa kwa kupitia Airtel Money Global Pay—kwa njia ya haraka, rahisi na salama.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Kampuni ya Telco EEMEA, Kirsten Wottman, ushirikiano wao na Airtel Money ni sehemu ya mkakati wa kupanua huduma za malipo salama kwa masoko yanayoendelea kama Tanzania, bila kujali kama mtumiaji ana akaunti ya benki au la.
“Ushirikiano wetu na Airtel Money unalenga kuhakikisha Watanzania, wanapata fursa ya kutumia njia salama kufanya miamala kidijitali zinazokubalika duniani kote kupitia Airtel Money Global Pay bila kujali wana akaunti ya benki au la. Uzinduzi huu unaonyesha dhamira yetu ya kuwawezesha Watanzania—wanafunzi, wafanyakazi wa mtandaoni, wasafiri, au wanunuzi—kushirikia katika uchumi wa kidigitali wa dunia. Lengo letu ni kuweka nguvu za kidijitali mikononi mwao, kwa usalama na uhakika.”
Jinsi ya Kupata Airtel Money Global Pay:
⦁ Pakua MyAirtel App kutoka Google Play au App Store
⦁ Chagua sehemu ya Airtel Money na ingia kwa kutumia PIN
⦁ Chagua Global Pay Card inayotumia Mastercard
⦁ Kubali vigezo na masharti
⦁ Jaza salio kutoka kwenye akaunti yako ya Airtel Money
⦁ Anza kutumia kadi yako kwenye tovuti mbalimbali za kimataifa.
0 Comments