Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania leo imeungana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika zoezi la usafi lililofanyika katika fukwe ya Kidimbwi, maarufu kama Kidimbwi Beach, iliyopo Kata ya Kawe, Mtaa wa Mbezi Beach B, Wilaya ya Kinondoni.
Zoezi hili ni sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofikia Juni 5, na linaendana na dhamira ya serikali ya kuzuia matumizi ya plastiki kwa kaulimbiu: "Pamoja Tutokomeze Taka za Plastiki."
Airtel pia imekabidhi vifaa vya usafi kwa uongozi wa Mtaa wa Mbezi Beach B ili kusaidia juhudi za kudumisha usafi wa mazingira kwa muda mrefu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Airtel Tanzania, Bi. Beatrice Singano, ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Udhibiti, alisema:
“Leo tumeungana na NEMC, Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, viongozi wa Mtaa wa Mbezi Beach B pamoja na wananchi kufanya usafi katika fukwe ya Kidimbwi ili kutokomeza taka za plastiki ambazo ni tishio kwa mazingira na viumbe wa baharini.”
Bi. Singano alisisitiza kuwa ni muhimu kwa jamii kubadili tabia na kupunguza matumizi ya plastiki kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo. Aliongeza kuwa Airtel inatathmini uwezekano wa kuweka utaratibu wa kudumu wa kufanya usafi katika fukwe mbalimbali nchini.
“Tunatambua kuwa viumbe wa baharini wana mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, hususan kupitia sekta ya uvuvi na utalii. Hivyo, ni wajibu wetu kuhakikisha mazingira yao yanabaki salama,” aliongeza.
Zoezi hilo limepokelewa kwa shangwe na wananchi wa eneo hilo ambao walishiriki kikamilifu, huku wakipongeza ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali katika kulinda mazingira.
0 Comments