Mbunge mstaafu wa muda mrefu wa Jimbo la Hanang’, Dkt. Mary Michael Nagu, amesema kwa moyo wa upendo na kujali aliouonyesha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Hanang’ wakati wa janga la maporomoko ya tope, mawe, maji na magogo kutoka Mlima Hanang’, wana Hanang’ hawatakuwa na budi bali kumlipa kwa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na Muungwana Blog Mjini Katesh, Dkt. Nagu alisema Rais Samia ameonyesha upendo wa dhati na kujitolea kwa hali na mali, akifanya kila linalowezekana kurejesha maisha ya wananchi waliokumbwa na janga hilo, hasa katika Kijiji cha Gendabi ambacho ndicho kilichoathirika zaidi.
“Rais Samia si tu alitufariji kwa maneno, bali ametekeleza kwa vitendo. Amefufua miundombinu ya barabara, umeme, maji na makazi. Hadi leo hii wananchi wameanza maisha mapya katika nyumba walizojengewa kwa msaada wa serikali yake. Hili ni deni la fadhila, na Wana Hanang’ lazima walipe fadhila hizo kwa kura za kishindo Oktoba,” alisema Dkt. Nagu.
Ameongeza kuwa hata nyumba yake binafsi iliyoko katika Kijiji cha Jorodom iliathiriwa na maporomoko hayo, lakini kupitia jitihada za serikali ya awamu ya sita, hali imeanza kurejea katika utulivu na usalama.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Samia. Taifa lipo salama, mkoa wetu wa Manyara unaendelea kufaidika na miradi ya maendeleo kila kona. Wana Manyara lazima waelewe kuwa huu ni wakati wa kumlipa mama yetu kwa kura,” alisisitiza.
Dkt. Nagu alitoa rai kwa wananchi wa Hanang’ na Manyara kwa ujumla kuendeleza mshikamano na kuunga mkono juhudi za serikali, akieleza kuwa maendeleo yanahitaji umoja, amani na uongozi wenye maono kama ule wa Rais Samia.
0 Comments