F KINNAPA yawarejesha Wanafunzi zaidi ya 200 masomoni. | Muungwana BLOG

KINNAPA yawarejesha Wanafunzi zaidi ya 200 masomoni.

Na John Walter -Babati

Wadau wa elimu nchini wametakiwa kuongeza juhudi na kupaza sauti zao ili kuwahamasisha wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali kurejea shuleni na kutumia fursa hiyo kutimiza ndoto zao.

‎Wito huo umetolewa na Mratibu wa Shirika la KINNAPA Development Programme, Abraham Akilimali, kupitia mradi wa Education Champion Network, ambao unalenga kuhamasisha uandikishaji mpya wa watoto wa kike waliokatisha masomo na kuwasaidia kupata elimu mbadala.

‎Akilimali amesema mradi huo umelenga zaidi jamii za wafugaji ili kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya msingi ya elimu.

‎Kwa mujibu wa Akilimali, katika wilaya ya Kiteto pekee, kwa mwaka 2024 wanafunzi 234 waliripotiwa kuacha shule.

‎Hata hivyo, kupitia jitihada za mradi wa Nipe Nafasi unaofadhiliwa na taasisi ya Malala, watoto zaidi ya 200 wamefanikiwa kurejea shuleni katika wilaya za Simanjiro, Kiteto, Babati, Siha na Hai.

‎Mradi huo pia umeunda zaidi ya klabu 20 mashuleni na kutoa mafunzo kwa viongozi wa mila, viongozi wa dini na maafisa elimu ili kuongeza uelewa na ushirikiano katika juhudi za kurejesha wanafunzi shuleni.

‎Katika mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari yaliyofanyika mjini Babati na kuhudhuriwa pia na maafisa ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Babati na Mkoa wa Manyara, Akilimali alisisitiza umuhimu wa kufuata muongozo uliotolewa na Wizara ya Elimu kuhusu madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto shuleni pamoja na mabaraza.

‎Alisema madawati hayo husaidia kutoa taarifa za vitendo vya ukatili, kuwajengea uwezo wanafunzi na walimu, na hivyo kusaidia watoto kutimiza malengo yao kielimu.

‎“Kila mmoja wetu katika jamii ana jukumu la kumlinda na kumsaidia mtoto ili asikatize masomo,” alisema Akilimali.

‎Kwa upande wake, Afisa Taaluma Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Mwalimu Judith Materu, alisema kati ya wanafunzi 85 waliokatisha masomo katika wilaya hiyo, tayari wanafunzi 21 wamerudi shuleni, wakiwemo wasichana 10 na wavulana 11 katika kipindi cha 2023 hadi 2025. 

Alibainisha kuwa kurejea shuleni kwa wanafunzi hao ni matokeo ya fursa iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

‎Naye Afisa Maendeleo wa Shirika la KINNAPA, Paulina Ngurumwa, ameiomba serikali kuongeza bajeti ya kuwawezesha wanafunzi wanaorejea shuleni na kuhakikisha viongozi wa mila na dini wanashirikishwa kikamilifu ili wawe mabalozi katika jamii zao kwa kuhamasisha watoto waliokatisha masomo.

‎KINNAPA imeendelea kutoa wito kwa jamii kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya pili ya kutimiza ndoto zake kupitia elimu.






Post a Comment

0 Comments