Na John Walter -Babati
Wananchi wapatao 18,652 wa kata ya Nkaiti katika tarafa ya Mbugwe, wilayani Babati mkoani Manyara wanatarajiwa kunufaika na huduma ya maji safi na salama kupitia mradi mpya wa ujenzi wa kituo cha kusukuma maji cha Mdori-Minjingu.
Mradi huu, unaotekelezwa na serikali kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Babati (BAWASA), una thamani ya shilingi milioni 921.58 na unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za magonjwa ya tumbo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakiwasumbua wakazi wa Nkaiti na maeneo jirani kutokana na kukosa chanzo cha uhakika cha maji safi.
Kwa mujibu wa Meneja wa Huduma kwa Wateja wa BAWASA, mradi unahusisha ujenzi na utandazaji wa mabomba makubwa ya maji kutoka eneo la chanzo hadi kwenye tangi lenye ujazo wa lita 250.
Akizungumza baada ya kukagua nyaraka na ubora wa ujenzi wa kituo hicho, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi, ameridhia kuweka jiwe la msingi na kuielekeza BAWASA kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili kuwanufaisha wananchi haraka iwezekanavyo.
Mradi huu ulianza kutekelezwa Aprili 24, 2025 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 30, 2025.
Baada ya kumaliza ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuendelea na ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kesho katika Halmashauri ya Mji wa Babati.
0 Comments