F Mwanafunzi afariki kwa kumeza puto alilokuwa analichezea. | Muungwana BLOG

Mwanafunzi afariki kwa kumeza puto alilokuwa analichezea.



Na John Walter-Babati

Mtoto Kelvin Nada mwenye umri wa miaka sita na miezi kumi, mkazi wa Kijiji cha Maganjwa wilayani Babati mkoani Manyara, amefariki dunia kwa madai ya kumeza puto (pulizo) wakati akicheza nyumbani kwao.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Maganjwa, Petro Shauri, tukio hilo la kusikitisha lilitokea siku ya Jumapili Julai 19, 2025, wakati mtoto Kelvin akiwa nyumbani kwao anacheza.

“Ni tukio la kusikitisha sana, mtoto Kelvin alikuwa anacheza nyumbani, ghafla akaanguka chini, Familia ilifanya jitihada kumpeleka hospitali, lakini kwa bahati mbaya alifariki njiani,” alisema Shauri.

Babu wa marehemu, Deengw Margwe slaa, amesema mtoto huyo alikuwa anachezea puto ambalo wanahisi alilimeza, kwani halikuonekana tena baada ya tukio hilo.

“Tulimkuta Kelvin ameanguka, na hatukuliona tena lile puto, tunaamini ndilo lilisababisha matatizo yake ya kupumua, alifariki dunia kabla hatujamfikisha hospitali ya Dareda Mission,” alisema kwa huzuni.

Kelvin Nada alikuwa mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Maganjwa. 

Akizungumzia kifo hicho, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Pius Noga, alisema wamepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa.

“Hili ni pigo kubwa kwetu kama walimu na wanafunzi wenzake, Kelvin alikuwa mtoto mchangamfu, mwenye bidii darasani, tunatoa pole kwa familia,” alisema Noga.

Mazishi ya Kelvin yamefanyika jana kijijini Maganjwa, huku wakazi wa eneo hilo wakielezea majonzi na huzuni kubwa kutokana na kifo hicho cha ghafla.

Tahadhari imetolewa kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanacheza na vitu salama, ili kuepusha madhara kama haya yasijirudie.

Post a Comment

0 Comments