Na John Walter -Kiteto
Mwenge wa Uhuru umefanya uzinduzi rasmi wa jengo jipya la zahanati katika Kijiji cha Ngabolo, Kata ya Ndedo, Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara.
Mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya shilingi 124,500,000 kutoka Serikali Kuu kupitia (WMA) Makame, pamoja na mchango wa shilingi 1,500,000 kutoka kwa wananchi wa Kijiji cha Ngabolo.
Awali, jengo hilo lililojengwa mwaka 2004 lilikuwa linahudumia wananchi wapatao 2,178.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya wakazi wa Kijiji cha Ngabolo imeongezeka na sasa inafikia watu 5,225, hivyo kufanya upanuzi na uboreshaji wa huduma kuwa jambo la lazima.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, Ismail Ussi, amepongeza usimamizi mzuri wa ujenzi huo na matumizi sahihi ya fedha, na hatimaye kuzindua rasmi jengo hilo jipya.
Ameeleza kuwa wananchi sasa watanufaika kwa kupata huduma za afya karibu na kuepuka vifo vitokanavyo na uzazi, hususan kwa watoto wachanga na akinamama wajawazito.
Katika tukio la kusisimua, Kiongozi huyo wa Mwenge wa Uhuru amekutana na mama aliyejifungua mtoto wa kiume usiku wa kuamkia leo katika zahanati hiyo, na kupendekeza mtoto huyo apewe jina la Ismail, jina lake, jambo ambalo limekubaliwa.
Aidha, Kiongozi huyo amempa mama huyo shilingi milioni tano ili zimsaidie kupata mahitaji muhimu kwa mtoto na familia.
Uzinduzi huo unaakisi dhamira ya serikali na wananchi kuimarisha huduma za afya na kuleta maendeleo endelevu katika maeneo ya vijijini.
0 Comments