Na John Walter-Babati
Mwenge wa Uhuru umeweka historia katika Halmashauri ya Mji wa Babati baada ya kuzindua majengo matano mapya katika Hospitali ya Mji huo, yaliyogharimu Shilingi Bilioni 1.4 kutoka serikali kuu kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Akizindua majengo hayo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amewataka watoa huduma katika hospitali hiyo kuhakikisha wanatoa huduma bora na kwa weledi, kulingana na maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali. Aidha, amempongeza Mganga Mkuu wa Mji wa Babati, Nasib Msuya, kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi huo.
Akisoma taarifa mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mganga Mkuu huyo alisema kuwa mradi huo umehusisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, maabara, jengo la mionzi, kichomea taka, jengo la kufulia pamoja na ujenzi wa njia za watembea kwa miguu.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza ubora wa huduma za afya, kupunguza vifo na kuwapunguzia adha wananchi wa Babati Mjini na maeneo jirani kupata huduma za afya bora kwa ukaribu.
Wananchi pamoja na uongozi wa hospitali hiyo wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma za afya nchini.
0 Comments