Na John Walter -Babati
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ali Ussi, amezindua mradi wa nishati mbadala katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Manyara wenye thamani ya shilingi milioni 21.9.
Mradi huo unalenga kurahisisha upikaji wa chakula kwa wanafunzi pamoja na kutunza mazingira kwa kupunguza ukataji miti ovyo.
Kiongozi huyo amesema ni jitihada za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya nchi na kulinda afya za Wananchi.
Akisoma taarifa kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa, Mkuu wa shule ya Manyara Girls, Bi. Gisella Msofe, amesema mradi huo wa gesi safi ya kupikia utapunguza muda wa kuandaa chakula na kuchangia jitihada za shule katika uhifadhi wa mazingira.
Baadhi ya wanafunzi akiwemo Sabrina Msangi, Faith Flavian na Sharon Msangi, wameishukuru serikali kwa mradi huo, wakieleza kuwa sasa watakuwa na muda zaidi wa kusoma badala ya kutumia muda mwingi kutafuta kuni, pamoja na kulinda afya zao kutokana na kupunguza moshi unaotokana na kuni na mkaa.
Mradi huo ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya mkaa na kuni ili kulinda mazingira, ambapo serikali imeanza na taasisi zinazolisha watu kuanzia 100 na imekuwa ikitoa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku ya shilingi 17,500.
0 Comments