F RC Manyara akabidhi chombo kwa RC Singida | Muungwana BLOG

RC Manyara akabidhi chombo kwa RC Singida


Na John Walter -Hanang'

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amemkabidhi rasmi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, baada ya Mwenge huo kukimbizwa mkoani Manyara kwa zaidi ya kilomita 1,000 ukipitia jumla ya miradi 51 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 71.3.

Katika mbio hizo za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, viongozi na wananchi wa Mkoa wa Manyara walionesha ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha miradi inayokaguliwa, kuzinduliwa au kuwekwa mawe ya msingi inatekelezwa kwa viwango vinavyokidhi thamani ya fedha na kuleta tija kwa wananchi.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2025, Ndg. Ismail Ali Ussi, alipongeza Mkoa wa Manyara kwa namna ulivyotekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa, akisisitiza kuwa juhudi hizo zinaonesha dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya sita ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.

Aidha, ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu ulisisitizwa kikamilifu katika kila halmashauri ya Mkoa wa Manyara, hususan ujumbe wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu, kama kaulimbiu ya mwaka huu inavyosema: “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.”

Akitoa taarifa wakati wa makabidhiano, mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema katika mapambano dhidi ya malaria, Mkoa wa Manyara umegawa zaidi ya vyandarua 100,000 kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuzuia maambukizi mapya ya ugonjwa huo hatari. 

Vilevile amesema, juhudi za kuboresha lishe bora zimeendelea kutekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya.

Kwa upande wa chanjo, Sendiga amesema watoto zaidi ya 300,000 wamepatiwa chanjo muhimu katika maeneo mbalimbali ya mkoa, ikiwa ni ishara ya mafanikio ya kampeni za afya ya msingi kwa watoto.

Sendiga amesema mkoa umeendelea na mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya ambapo jumla ya kete za bangi 4,644 na mirungi kilo 322,000 zimekamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda kizazi kijacho dhidi ya madhara ya matumizi ya dawa hizo haramu.

Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chombo muhimu cha kuhamasisha maendeleo, umoja, amani na mshikamano wa kitaifa, huku Mkoa wa Manyara ukionesha mfano wa kuigwa kwa utekelezaji mzuri wa miradi na ushirikiano wa viongozi na wananchi katika kuhakikisha mafanikio ya taifa yanapatikana kwa vitendo.

Post a Comment

0 Comments