Na John Walter-Babati
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amepiga marufuku viongozi na watumishi wa umma mkoani humo kujilimbikizia mali ambazo wanashindwa kuziendeleza, akieleza kuwa hali hiyo inaziba fursa kwa wananchi wengine kupata maendeleo.
Sendiga alitoa agizo hilo Julai 24, 2025, wakati wa hafla ya kumkabidhi mkandarasi eneo la ujenzi wa stendi ya mabasi, barabara za lami na mitaro katika stendi ya muda ya Makatanini, mjini Babati.
Amesema baadhi ya viongozi wamekuwa wakijipatia mali nyingi – zikiwemo vibanda – lakini wanashindwa kuviendeleza, hali inayokwamisha matumizi bora ya rasilimali zilizopo kwa manufaa ya jamii.
“Marufuku kujilimbikizia vibanda vitakavyojengwa katika stendi hii mpya. Kila mmoja apate kibanda kimoja ili kutoa nafasi kwa wengine, wale waliopo sasa kwenye stendi ya muda wapewe kipaumbele kwa gharama nafuu,” alisisitiza.
Aidha, alibainisha kuwa kukamilika kwa stendi hiyo kutachangia kukuza uchumi wa wananchi wa Babati na kuondoa kero ya vumbi ambalo limekuwa likisababisha maradhi kwa watumiaji wa stendi hiyo kwa muda mrefu.
Kwa upande mwingine, Mkuu huyo wa Mkoa alimwagiza mkandarasi anayetekeleza mradi huo, kampuni ya Wesons Engineers, kuhakikisha hakuna visingizio vya kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo na kwamba kazi ifanyike kwa ubora na ikamilike kwa wakati.
“Tunataka kuona thamani ya fedha kwenye kila senti, hakuna sababu ya kuchelewa au kutoa visingizio. Ujenzi uende kwa kasi na ubora unaotakiwa,” alisema Sendiga.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 15 kwa gharama ya shilingi bilioni 19.996, na unahusisha ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 4.7 pamoja na mitaro ya kupitisha maji yenye urefu wa kilomita 8.15.
Ujenzi wa stendi hiyo mpya unatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa sekta ya usafirishaji mjini Babati na kuchochea biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.
0 Comments