Na John Walter -Babati
Zoezi la kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi za udiwani na ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Manyara limekamilika leo, Julai 2, 2025, saa kumi kamili jioni.
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo ya Ufundi wa CCM mkoa wa Manyara, John Zwalile, ambaye amesema jumla ya wagombea 82 wamechukua na kurejesha fomu kwa wakati katika kipindi cha siku tano kuanzia Juni 28 hadi Julai 2, 2025.
Kwa mujibu wa Zwalile, idadi ya waliorejesha fomu kwa kila wilaya ni kama ifuatavyo:
Babati Mjini – 17 (wanawake 4)
Babati Vijijini – 11 (wanawake 2)
Kiteto – 9 (wanawake 2)
Hanang' – 12 (wanawake 3, wakiwemo Mbunge wa Vijana Asia Halamga)
Mbulu Vijijini – 9 (wanawake 2)
Mbulu Mjini – 5 (wanaume pekee)
Simanjiro – 15 (wanawake 5)
Zwalile amesema hakuna malalamiko yaliyopokelewa kuanzia ngazi ya kata wakati wa zoezi hilo, jambo linalodhihirisha uelewa na utulivu miongoni mwa wanachama.
Aidha, mchakato wa kuchuja majina ya wagombea utaendelea kama ifuatavyo:
Julai 4, 2025 – Ngazi ya kata
Julai 6, 2025 – Ngazi za wilaya
Julai 7, 2025 – Ngazi za jumuiya
Zwalile ametoa wito kwa wanachama wote kuendelea kushiriki kwa amani na utulivu hadi kukamilika kwa mchakato mzima wa ndani ya chama.
Kwa idadi hiyo 82 ya watia nia ina maanisha kuwa wamekichangia Chama shilingi milioni 41 kwa kulipia shilingi laki tano kwa fomu, hiyo ni kwa majimbo pekee tofauti na zile za wawakilishi wa mkoa kupitia jumuiya mbalimbali za Chama cha Mapinduzi.
0 Comments