Na John Walter-Simanjiro
Mwenyekiti wa shirika la ECLAT Development Foundation, Peter Toima, na Mwenyekiti wa Upendo Association ya nchini Ujerumani, Dk. Fred Heimbach, wamekabidhiwa tuzo ya heshima na wananchi wa Kata ya Msitu wa Tembo, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.
Tuzo hizo zimetolewa kutokana na mchango wao mkubwa katika sekta ya elimu si tu kwa kata hiyo, bali pia kwa Wilaya ya Simanjiro na taifa kwa ujumla.
Hafla ya kukabidhi tuzo hizo ilifanyika katika Shule ya Sekondari Msitu wa Tembo, mara baada ya ECLAT Foundation kukabidhi bweni jipya la wasichana lililojengwa kwa gharama ya shilingi Milioni 210 na kukamilishwa kwa vifaa vyote muhimu ikiwemo vitanda, magodoro, huduma ya maji, umeme, vyoo na sehemu za kunawia mikono.
Tuzo hizo zilikabidhiwa rasmi na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Makota, akiwapongeza wadau hao kwa jitihada za dhati katika kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha elimu.
Mbali na viongozi hao wawili, tuzo ya heshima pia ilitolewa kwa Bakir Angalia, Meneja Miradi wa ECLAT Development Foundation, kwa mchango wake katika uratibu wa miradi ya maendeleo inayoendelea kunufaisha jamii ya Simanjiro.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo, Toima alisema heshima hiyo inawatia moyo kuendelea kushirikiana na jamii katika kuendeleza sekta ya elimu na huduma za kijamii.
Aidha, aliwahimiza wananchi kushirikiana katika kulinda na kuthamini miundombinu iliyopo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Peter Toima, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, ameahidi kuendelea kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali ili kuhakikisha elimu inakuwa chachu ya maendeleo katika mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.
Picha mbalimbali wakati wa makabidhiano ya tuzo.Picha na John Walter 






