Afande Fatuma Silaa awaasa wanafunzi kuepuka vijizawadi vinavyoharibu ndoto zao


Na John Walter-Babati

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Babati, Afande Fatuma Silaa, ametoa wito kwa wanafunzi kuepuka kupokea vijizawadi kutoka kwa watu wasiowajua akisisitiza kuwa zawadi hizo mara nyingi huwa chanzo cha kuharibiwa ndoto na mustakabali wa maisha yao.

Akizungumza na wanafunzi wa shule za sekondari Dabil na Maganjwa, Afande Silaa aliwahimiza kuripoti mara moja vitendo vyote vya ukatili wanavyofanyiwa, kusikia au kushuhudia.

Alibainisha kuwa taarifa zinaweza kutolewa kwa mwenyekiti wa kijiji, viongozi wa dini, polisi au kwa kupiga namba ya bure 116 ili hatua zichukuliwe haraka dhidi ya wahusika.

Amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia ni chanzo cha kurudisha maendeleo nyuma na kuvunja ndoto za watoto pamoja na watu wazima. 

Kupitia elimu hiyo, wanafunzi walipatiwa uelewa kuhusu maana ya ukatili wa kijinsia, aina zake, sababu zinazochangia, maeneo ya kuripoti na hatua za kuchukua baada ya kutendewa ukatili. 

Aidha, Afande Silaa aliwatahadharisha wanafunzi kuhusu matumizi mabaya ya simu za mkononi akisema yamekuwa sehemu ya kuchochea ukatili huo.

Aliwataka Wanafunzi kutumia simu kwa ajili ya kujifunza na kuimarisha elimu badala ya matumizi yasiyo na tija.


Picha zote na John Walter-Babati












Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items