F Msitu wa Tembo wapata bweni jipya la kisasa kwa wanafunzi wa kike. | Muungwana BLOG

Msitu wa Tembo wapata bweni jipya la kisasa kwa wanafunzi wa kike.


Na John Walter-Simanjiro

Wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Msitu wa Tembo, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamepata faraja kubwa baada ya kukabidhiwa bweni jipya la kisasa lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120. 

Hatua hiyo inatarajiwa kuondoa changamoto ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kila siku na kukabiliana na vishawishi njiani vilivyokuwa vikikatisha ndoto za baadhi yao za kupata elimu.

Bweni hilo lililogharimu shilingi milioni 210 limejengwa na ECLAT Development Foundation kwa kushirikiana na Upendo Association ya Ujerumani, likiwa na vitanda na magodoro 120, vyoo 10 vikiwemo vya wanafunzi wenye mahitaji maalum, sehemu za kufulia pamoja na huduma muhimu za umeme na maji safi.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mwenyekiti wa ECLAT Development Foundation ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima, alisema bweni hilo ni chachu ya maendeleo ya elimu kwa watoto wa kike na kwamba jamii nzima inapaswa kushirikiana kuhakikisha wanafunzi wanatumia ipasavyo fursa waliyoipata.

“Elimu ni ufunguo wa maisha, kila mmoja anatakiwa kuupata,  ni msingi wa maendeleo na kumaliza migogoro kwa kuwa wasomi sio watu wa migogoro. Elimu ni kitu cha thamani na cha kukumbatiwa,” alisema Toima.

Meneja Miradi wa ECLAT, Bakir Angalia, alisema mradi huo umetokana na mahitaji makubwa ya shule hiyo ambapo awali wanafunzi walilazimika kulala chini kwa kubanana kwenye bweni dogo.

“Tuliona changamoto kubwa kwa watoto wa kike, tukasema lazima tutoe suluhisho. Hili bweni ni matunda ya mshikamano wa wadau wa maendeleo na linaenda kuandika historia mpya katika Msitu wa Tembo,” alisema Angalia.

Bweni hilo limepewa jina la “GLORIA”, kwa heshima ya Mkuu wa Shule ya Sekondari Msitu wa Tembo, Gloria Sizia, kutokana na jitihada zake kubwa za kupigania mradi huo.

Katika risala yao, wanafunzi kupitia mwakilishi wao Naomi Rajabu, walieleza kufurahishwa na bweni hilo la kisasa na kuahidi kutumia fursa hiyo kusoma kwa bidii. 

Hata hivyo, wanafunzi wa kiume nao waliomba kujengewa bweni ili nao wapunguzwe adha ya kutembea umbali mrefu kila siku.

Mkuu wa shule hiyo, Gloria Sizia, alishukuru ECLAT na wadau wote waliosaidia mradi huo, akibainisha kuwa bweni litapunguza changamoto nyingi zilizokuwa zikitatiza elimu ya watoto wa kike.

Naye, Mwenyekiti wa Upendo Association ya nchini Ujerumani, Dk. Fred Heimbach, aliahidi kuendelea kushirikiana na ECLAT kuhakikisha jamii za pembezoni zinapata mazingira bora ya elimu.

“Elimu ndiyo kila kitu. Tutashirikiana kuhakikisha watoto wote, hususani wa vijijini, wanapata nafasi sawa ya kusoma kama wenzao wa mijini,” alisema Dk. Heimbach.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota, aliishukuru ECLAT Development Foundation kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha elimu, akisema taasisi hiyo imekuwa mdau muhimu wa maendeleo na inastahili pongezi.

Nao baadhi ya  Wazazi walioshuhudia hafla ya makabiadhiano ya bweni hilo, wamesema hatua hiyo ni  ukombozi mkubwa kwao na jamii ya Msitu wa Tembo waliokuwa wakishuhudia watoto wao wakihangaika kwa miaka mingi kutokana na ukosefu wa mabweni bora.


Picha mbalimbali, na John Walter



















Post a Comment

0 Comments