Na John Walter- Simanjiro
Shule mpya ya Msingi Ole Mbole iliyojengwa katika Kata ya Komolo, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, imekabidhiwa rasmi kwa serikali baada ya kukamilika kwa ufadhili wa Shirika la ECLAT Development Foundation kwa kushirikiana na Upendo Association pamoja na 1000 Schulen für unsere Welt la nchini Ujerumani.
Shule hiyo imegharimu shilingi Milioni 169.2, ikiwa na madarasa mawili, ofisi ya walimu, nyumba moja ya mwalimu, matundu ya vyoo 32 pamoja na madawati na meza za wanafunzi.
Mwenyekiti wa ECLAT na CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima, ndiye aliyeongoza hafla ya makabidhiano hayo na kukabidhi shule hiyo kwa Serikali ya Wilaya ya Simanjiro.
Afisa Elimu Msingi wa Wilaya hiyo alipokea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya.
Katika hafla hiyo, wananchi wa Komolo walimshukuru Toima na kumzawadia ndama dume wa ng’ombe kama ishara ya kutambua mchango wake katika kufanikisha mradi huo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Komolo, Ndikoya Siara, alisema awali watoto walikuwa wanatembea zaidi ya kilomita nane kufuata shule nyingine na kubanana madarasani.
“Shule hii imetupunguzia kero kubwa, tunaomba kuongezewa madarasa zaidi kwa sababu mahitaji bado ni makubwa,” alisema.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Wilaya, Marco Masala, alisema ECLAT ni mfano wa mashirika yanayoweza kuleta mwamko wa elimu katika jamii za kifugaji ambazo awali zilikuwa zikikabiliwa na changamoto ya kutowapeleka watoto shule.
Naye Mwenyekiti wa Upendo Association, Fred Heimbach, alisema furaha yao kubwa ni kuona watoto wa jamii za kifugaji wakipata elimu badala ya kuishia kuchunga mifugo.
Akizungumza baada ya kukabidhi shule hiyo, Toima aliwashukuru wafadhili na kuahidi kuendelea kutafuta rasilimali zaidi kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Ni wajibu wa wazazi sasa kupeleka watoto shule na kuachana na mila zilizopitwa na wakati zinazokwamisha elimu ya watoto,” alisema.
Kwa kukamilika kwa ujenzi huo, Kijiji cha Komolo sasa kitakuwa na shule mbili za msingi – Komolo na Ole Mbole – baada ya kusajiliwa rasmi.