Wazazi, Walimu Waaswa Kuwalinda Watoto Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia


Na John Walter-Babati

Wazazi, walezi na walimu wametakiwa kuwa karibu na watoto wao ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wanaishi kwa usalama. 

Wito huo umetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Goodman, wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Sora juu ya aina mbalimbali za ukatili na mbinu za kuuepuka.

Aidha, Afisa wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Manyara, Stella Bagega, amewashauri watoto na wazazi kuhakikisha wanatoa taarifa pindi wanaposhuhudia au kufanyiwa ukatili kwa kuwasiliana na dawati la jinsia na watoto la polisi au kupiga namba ya bure 116 ili kupata msaada wa haraka.

Kwa upande wake, Rose Kalage kutoka Shirika la Haki Elimu akishirikiana na Marafiki wa Elimu Babati kupitia programu ya Elimika, Elimisha, Wajibika Kumlinda Mtoto wa Kike, amewataka wazazi kuepuka kutumia muda mwingi kwenye simu na badala yake wawe karibu na watoto wao ili kuwalea na kuwalinda dhidi ya mazingira hatarishi.

Shughuli hiyo ya kutoa elimu shule za msingi na Sekondari pamoja na walimu, imelenga kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu wajibu wa pamoja wa kumlinda mtoto, hasa wa kike, dhidi ya ukatili na unyanyasaji.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items