Waandishi wa habari nchini wametakiwa kutumia kalamu zao kwa uangalifu na weledi mkubwa hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kwa kuzingatia uandishi unaozingatia ukweli na maslahi ya Taifa.
Akizungumza katika mafunzo ya waandishi wa habari yanayofanyika jijini Arusha, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Rodney Mbuya, alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuelimisha jamii na kuimarisha demokrasia, hivyo vinapaswa kuepuka uandishi wa kupotosha au kuchochea migawanyiko.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa AICC yameandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga wameshiriki.
Mgeni rasmi katika mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kalli, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, aliwataka wanahabari kuhakikisha wanazingatia maadili na uandishi wa kitaaluma.
“Waandishi wa habari ni daraja muhimu kati ya Serikali na wananchi, lazima mtoe taarifa sahihi kupitia vyanzo sahihi ili kusaidia umma kufanya maamuzi yenye tija,” alisema.
Mafunzo hayo yamelenga kuwaandaa waandishi wa habari katika kuripoti kwa ufanisi na uadilifu kipindi cha kampeni na uchaguzi mkuu ujao.
