Na John Walter-Manyara
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara imepitia mapendekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025–2030, katika kikao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Mheshimiwa Peter Toima.
Katika kikao hicho kilichofanyika kwa mujibu wa maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wajumbe walijadili na kuweka bayana vipaumbele vya chama kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele ni Afya, Elimu, Barabara, Maji, Ufugaji, Uvuvi, Kilimo, Ustawi wa Jamii, Michezo pamoja na Mawasiliano.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Mh. Peter Toima, alisema chama hicho katika mkoa huo kitaendelea kushinda kwa kishindo na kusimamia utekelezaji wa ilani hiyo kwa vitendo.
Wazee maarufu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo waliokuwa miongoni mwa washiriki, walionesha kuridhishwa na masharti ya Ilani mpya hususan maeneo yanayogusa moja kwa moja Mkoa wa Manyara.

Hata hivyo, walitoa ushauri kwa chama kuhakikisha mikakati ya kulinda tunu muhimu za mkoa huo inaimarishwa.
Miongoni mwa tunu walizozitaja ni pamoja na madini adhimu ya Tanzanite, mashamba makubwa ya ngano ya Basotu wilayani Hanang, pamoja na utamaduni, mila na desturi za makabila ya mkoa huo hususan ya Wahadzabe.
Kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Manyara ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030, ambapo kila mkoa umeagizwa kuchanganua maeneo ya kipaumbele kulingana na hali na rasilimali zilizopo.

