F Mkuu wa mkoa Manyara alaani mauaji ya mwanafunzi Qash | Muungwana BLOG

Mkuu wa mkoa Manyara alaani mauaji ya mwanafunzi Qash



Na John Walter-Babati

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amelaani vikali tukio la kikatili lililosababisha kifo cha mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Qash, wilayani Babati, Yohana Amani Konki (17), baada ya kushambuliwa na wanafunzi wenzake kwa tuhuma za wizi wa simu.

Akizungumza mara baada ya kupata taarifa za tukio hilo, RC Sendiga amelielezea kama ni tendo la kinyama, linalotokana na imani potofu na tabia ya wananchi kujichukulia sheria mikononi badala ya kufuata taratibu za kisheria.

Ameagiza jeshi la polisi kumsaka na kumfikisha katika vyombo vya sheria mganga wa kienyeji anayedaiwa kutumia ramli kudai kuwa marehemu ndiye aliyeiba simu (tablets) iliyokuwa imepotea.

“Ni lazima mganga huyu akamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria, kwa sababu imani potofu kama hizi zinachochea mauaji na kuathiri jamii yetu,” alisema RC Sendiga.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mazingira ya shule zote zenye wanafunzi wanaoishi hosteli, ili kubaini kama kulikuwa na uzembe wowote katika tukio hilo na kuchukua hatua dhidi ya wahusika.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Qash, Sosi Abdala, tukio hilo lilitokea alfajiri ya Agosti 16, 2025, baada ya mganga huyo kudai kwa kutumia ramli kuwa Yohana ndiye aliyeiba simu hiyo.

Taarifa zinasema kuwa wanafunzi 12 walihusishwa katika shambulio hilo, ambapo walimvamia na kumpiga marehemu hadi kusababisha kifo.

Wananchi wa eneo hilo wameelezea masikitiko yao makubwa kutokana na tukio hilo, wakitoa wito wa kuchukuliwa hatua kali kwa wote waliohusika ili iwe fundisho kwa wengine.

Hata hivyo tayari wanafunzi 11 wanashikiliwa kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo, huku uchunguzi wa awali ukionyesha kuwa chanzo kikuu ni imani za kishirikina pamoja na kutokuwepo uthibitisho wa kisheria.

Post a Comment

0 Comments