F CCM Yakusanya Bilioni 56.31 katika Harambee ya Uchaguzi Mkuu 2025. | Muungwana BLOG

CCM Yakusanya Bilioni 56.31 katika Harambee ya Uchaguzi Mkuu 2025.



Na John Walter-Babati

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanikisha kukusanya jumla ya shilingi bilioni 56.31, pamoja na ahadi za kuchangia kiasi cha shilingi bilioni 30.2, katika harambee maalum ya kuchangia shughuli za kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Harambee hiyo imefanyika leo katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Samia amewashukuru wote waliotoa michango yao kwa moyo wa upendo na mshikamano, akisisitiza kuwa chama hicho kikongwe chenye historia kubwa ya kuongoza taifa kinahitaji kutunzwa na kulishwa ili kiendelee kudumu kwa manufaa ya wananchi.

“Kazi na utu, tunasonga mbele, Chama chetu kimekuwa msingi mzuri wa muungano, mshikamano wa wanachama na vitendo ndivyo vitakavyokipeleka mbele. Kutoa ni moyo na sio utajiri,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake katibu mkuu wa CCM Dkt Emmanuel  Nchimbi amesema zoezi la uchangiaji linaendelea na malengo ni kukusanya bilioni 100 ili kufanikisha maandalizi yote ya kampeni za chama kwa mwaka huu.

Fedha zilizopatikana zinatarajiwa kusaidia CCM kuzunguka nchi nzima kuomba ridhaa ya wananchi kuendelea kuongoza taifa.

Post a Comment

0 Comments