F Kampeni ya "Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa" Yaendelea Awamu ya Pili Babati | Muungwana BLOG

Kampeni ya "Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa" Yaendelea Awamu ya Pili Babati

Na John Walter Babati.

Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi Wilaya ya Babati limeendelea na utekelezaji wa kampeni ya “Tuwaambie kabla hawajaharibiwa” awamu ya pili, kwa kutoa elimu kwa wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Komoto, Halmashauri ya Mji wa Babati, mkoani Manyara.

Mkuu wa Dawati hilo, Mkaguzi wa Polisi Fatuma Silaa, amesema kampeni hiyo inalenga kuwalinda watoto wa kike na wa kiume wanaotarajia kuhitimu elimu ya msingi na sekondari, ili wanapokutana na changamoto za maisha ya mtaani waweze kujilinda na kuepuka hatari zinazoweza kuharibu ndoto zao.

Ameeleza kuwa mada zilizotolewa ni pamoja na elimu ya ukatili wa kijinsia, namna ya kuripoti vitendo vya ukatili, aina za ukatili, maadili mema na uzalendo.

“Jamii imeanza kuharibika kutokana na vitendo vya ukatili na mmomonyoko wa maadili, hivyo ni wajibu wetu kuongeza jitihada kubwa kuwaelimisha watoto ambao ndiyo taifa la kesho,” alisema Mkaguzi Silaa na kusisitiza kuwa vitendo vya ukatili havina nafasi katika jamii.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Komoto, Evaline Aremu, amepongeza Dawati la Jinsia na Watoto kwa kutoa elimu hiyo muhimu akisema inawajenga wanafunzi kujitambua na kuwa na msimamo imara wanapokabiliana na changamoto za maisha.

Nao baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba waliohudhuria mafunzo hayo wamesema elimu hiyo iwafikie mara kwa mara kwani inawakumbusha namna ya kujilinda na kuendelea kufanikisha ndoto walizonazo.

Post a Comment

0 Comments