KITETO: Mamia Wamiminika Kumsikiliza Mbunge Edward Ole Lekaita



Na John Walter -Kiteto

Mamia ya wakazi wa Wilaya ya Kiteto wamekusanyika katika Kata ya Sunya kushiriki uzinduzi wa kampeni za Mbunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wakili Edward Ole Lekaita.

Wananchi waliohudhuria mkutano huo wamesema wana imani kubwa na kiongozi huyo kutokana na kazi kubwa alizofanikisha katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. 

Wameeleza kuwa Ole Lekaita amesaidia kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji, kujenga madaraja maeneo yaliyokuwa hayapitiki, pamoja na maboresho kwenye sekta za afya, maji, elimu na miradi mingine ya maendeleo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Ole Lekaita amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 150 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Jimbo la Kiteto, kiwango ambacho hakijawahi kutolewa hapo awali. 

Miongoni mwa mafanikio hayo ni ujenzi wa shule mpya tano za sekondari, shule shikizi 18, shule za mfano, pamoja na vituo vitatu vipya vya afya.

“Kiteto tutahakikisha tunampatia kura nyingi za ndiyo ifikapo Oktoba 29 kwa Rais wetu Dkt. Samia,” amesema Ole Lekaita huku akisisitiza kuwa ataendelea kutembelea wananchi kusikiliza na kutatua changamoto zao.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Manyara, Christina Masagasi, aliwataka wana CCM kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 na kila mmoja kupeleka angalau wapiga kura watatu zaidi.

Wilaya ya Kiteto yenye jumla ya kata 23 pia inashuhudia ushiriki wa mgombea mwanamke pekee wa ubunge kupitia CCM, Theresia Chibago, kutoka Kata ya Engusero anayewania kwa awamu ya pili.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kiteto Hassan Losioki alifungua rasmi kampeni hizo kwa kumtambulisha mgombea ubunge Edward Ole Lekaita na kumsifu kama kiongozi mwenye hekima na mpenda maendeleo.

Shughuli hiyo ilipambwa na burudani mbalimbali zilizowasisimua wananchi waliojitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo wa kampeni.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi