Kiteto wajipanga kuipa CCM kura nyingi Oktoba 29

Na John Walter -Babati

Mgombea ubunge jimbo la Kiteto Wakili Edward Ole Lekaita amesema wakazi wa Kiteto wameonesha mapenzi makubwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu kura za maoni, ambapo alifanikiwa kushika nafasi ya pili kitaifa kwa kupata kura nyingi.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za CCM mkoa wa Manyara uliofanyika Septemba 6, 2025, katika uwanja wa Motel Papaa mjini Babati na kuhudhuriwa na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Hamad Chande, mgombea huyo alisema Oktoba 29 wakati wa uchaguzi mkuu ndiyo itakuwa kilele cha ushindi wa chama hicho.

“Tunataka kuongoza kitaifa kwa kuipa CCM kura nyingi, Wana Kiteto waliojiandikisha kupiga kura ni laki mbili na elfu kumi na tano mia mbili sitini na mbili, naamini wote watatupa kura,” alisema.

Aidha, alitaja miradi mikubwa ya maendeleo iliyotekelezwa Kiteto ikiwemo ujenzi wa sekondari tano mpya, shule 20 za msingi, vituo vya afya vitatu vipya, na chuo cha ufundi stadi (VETA) kwa mara ya kwanza wilayani humo. 

Pia alisema vijiji vyote vimepatiwa umeme na maji.

“Kabla tulikuwa na upatikanaji wa maji kwa asilimia 37 pekee, lakini sasa tunazungumzia asilimia 87, hii ni kazi kubwa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tuna deni kubwa la kuhakikisha kura nyingi zinakwenda CCM Oktoba 29,” alisisitiza.

Uzinduzi huo wa kampeni uliambatana na shamrashamra kubwa huku viongozi mbalimbali wa chama na wananchi wakihamasishwa kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi