Na John Walter-Babati
Uzinduzi rasmi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Manyara kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, umefanyika septemba 6,2025 katika viwanja vya Motel Papaa mjini Babati, na kuvuta mamia ya wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio hilo.
Akihutubia wananchi, Hamad Chande, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, amesema mafanikio makubwa yaliyofanikishwa na Rais na Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanapaswa kuwa kichocheo kwa kila Mtanzania kujitokeza kupiga kura kwa chama hicho kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais.
Chande amewaombea kura wagombea wote wa CCM katika mkoa wa Manyara na kutoa wito kwa wananchi kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu ili kuhakikisha maendeleo endelevu yanaendelea kupatikana nchini.
Aidha, amewanadi wagombea wa ubunge katika majimbo saba ya Manyara ambao ni:
-
Daniel Sillo (Babati Vijijini)
-
Emmanuel Nuwas (Mbulu Vijijini)
-
Asia Halamga (Hanang’)
-
James ole Millya (Simanjiro)
-
Emmanuel Qambay (Babati Mjini)
-
Wakili Edward Ole Lekaita (Kiteto)
Zacharia Isaay (Mbulu Mjini)
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima, amesema chama hicho kina uhakika wa kushinda kwa kishindo katika majimbo yote saba ya ubunge, kata 142 na nafasi za madiwani viti maalum zaidi ya 27.
Amesisitiza kuwa wananchi wa Manyara wameendelea kuthamini na kuunga mkono CCM kutokana na kazi nzuri ya maendeleo na uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa heshima ya chama hicho imeendelea kulindwa na kuimarishwa.
Toima amehitimisha kwa kusema: “Mkoa wa Manyara hauna chama kingine zaidi ya CCM, wananchi wanaamini katika kazi na uongozi wa chama chetu.”

