F Manyara Yazindua Kampeni kwa Kishindo, Yajipa Uhakika wa Ushindi Oktoba 29. | Muungwana BLOG

Manyara Yazindua Kampeni kwa Kishindo, Yajipa Uhakika wa Ushindi Oktoba 29.



Na John Walter-Babati
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Peter Toima, amesema chama hicho kimejipanga kufanya kampeni kila kona ya mkoa huo ili kuhakikisha kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM mkoani Manyara uliofanyika Septemba 6, 2025, katika uwanja wa Motel Papaa mjini Babati, Toima alisisitiza kuwa hakuna shaka kuwa mgombea urais wa CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, atapata kura nyingi za ushindi sambamba na wabunge na madiwani wa chama hicho.

“Tunakwenda kufanya kampeni kila kona ya mkoa huu, na nina uhakika Rais wetu Dkt. Samia, wabunge na madiwani wote wa CCM watapata kura za kutosha. Manyara hauna chama kingine zaidi ya CCM, wananchi wanaamini katika kazi na uongozi wa chama chetu,” alisema Toima.

Aidha, Mwenyekiti huyo alieleza kuwa CCM ina uhakika wa kushinda majimbo yote saba ya ubunge, kata 142 pamoja na zaidi ya viti 27 vya madiwani wa viti maalum. Aliongeza kuwa wananchi wa Manyara wameendelea kuthamini na kuunga mkono CCM kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na uongozi bora wa Rais Dkt. Samia.

Kwa upande wake, mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Hamad Chande, aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, aliwataka wanachama na wananchi wa Manyara kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 na kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi ili kuendeleza maendeleo yaliyopatikana.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, wabunge, madiwani, pamoja na mamia ya wananchi wa mkoa wa Manyara waliokusanyika kushuhudia tukio hilo lenye shamrashamra kubwa.

Post a Comment

0 Comments