Na John Walter-Babati
Kampuni ya Mati Super Brands ltd kupitia taasisi yake ya Mati foundation, imeanza rasmi mradi wa kukabidhi pikipiki za magurudumu matatu zinazotumia nishati ya umeme kwa watu wenye ulemavu nchini ili kuwasaidia kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa ufanisi zaidi.
Hafla ya makabidhiano imeongozwa na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo David Mulokozi ambaye ameeleza kuwa watu wenye mahitaji maalumu katika jamii hasa wale wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kuingiza kipato wanahitaji kuwezeshwa kwa miundombinu bora ili waweze kuchangia uchumi wa taifa kupitia shughuli wanazozifanya.


"Tumekabidhi pikipiki kwa ajili ya ndugu zetu wenye ulemavu hasa wale wanaojishughulisha ili ziwasaidie katika shughuli zao na wasaidie katika kujenga uchumi wa taifa letu". Alisema Mulokozi
Baadhi ya wanufaika wa vyombo hivyo vya usafiri ambao ni watu wenye ulemavu wanaojishugulisha, Bi Aisha Wenga na Ramadhani Biyeda kutoka katika wilaya ya Babati wameishukuru 'Mati foundation' kwa kugusa maisha ya jamii yenye makundi maalumu wakieleza kuwa jitihada hizo zinakwenda kuleta chachu na kuongeza ufanisi katika shughuli zao.


"Nimekuwa napoteza pesa na muda nikiwa nafuatilia madeni kwa ajili ya biashara yangu ya mahindi,Sasa kwa pikipiki hii itasaidia kufanya kazi zangu''.Alisema Ramadhani.
Meneja mradi wa mati foundation Isack Piganio amesema taasisi hiyo ikishirikiana na Mati Super Brands imekuwa ikijitolea kurudisha kwa jamii sehemu ya faida yake, huku mradi huu wa ugawaji pikipiki za magurudumu matatu ukiwa ni miongoni mwa miradi mingine ambayo wameendelea kuifanya.
Taasisi hiyo imeeleza mpango wake wa kutoa pikipiki zaidi ya 2000 kwa makundi ya watu maalumu ili kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili katika shughuli za utafutaji.



