Na John Walter-Singida
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Singida imewataka watu wenye ulemavu kutoa ushirikiano wa karibu kwa taasisi hiyo pale wanapobaini vitendo vya rushwa, hususan kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Kauli hiyo imetolewa na Onesmo Mdegela, aliyemwakilisha Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Singida, wakati akifungua semina maalum kwa watu wenye ulemavu iliyolenga kudhibiti vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi huo.
“Hakika nyinyi ni watu wenye mchango mkubwa sana kwenye jamii, hivyo tukaona ni vyema tuwashirikishe kwa kuwapatia elimu ya kupambana na rushwa hasa kipindi cha uchaguzi mkuu,” alisema Mdegela.
Aidha, alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa hayapaswi kuishia kwenye kipindi cha uchaguzi pekee, bali washiriki wa mafunzo hayo wanapaswa kuyatumia kama nyenzo ya kuzuia vitendo vya rushwa kwenye jamii zao za kila siku.
Kwa upande wao, washiriki wa semina hiyo ambao ni watu wenye ulemavu waliishukuru TAKUKURU kwa kuwakumbuka na kuwashirikisha, wakieleza kuwa ni mara ya kwanza kushirikishwa moja kwa moja na taasisi hiyo.

Wameiomba TAKUKURU kuendelea kuwafikia makundi mengine ya jamii nchini ili elimu ya kupambana na rushwa iweze kuwafikia Watanzania wote, hatua itakayosaidia kutokomeza vitendo vya rushwa kwa ujumla.

