RC Manyara awataka viongozi kutumia hekima kusikiliza kero za wananchi


Na John Walter -Manyara

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amewataka viongozi na watumishi wa serikali mkoani humo kutumia hekima na busara katika maamuzi yao, hususan wanaposhughulikia changamoto zinazowasilishwa na wananchi.

Sendiga ametoa kauli hiyo leo Septemba 10, 2025, wakati wa Baraza Maalum la kusikiliza kero za wananchi kutoka wilaya mbalimbali za mkoa huo, lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa.

Katika kikao hicho, RC Sendiga amesikiliza malalamiko mbalimbali, mengi yakiwa ni ya migogoro ya ardhi na ya kifamilia, na kusisitiza umuhimu wa familia kuishi kwa kupendana ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.

Aidha, amewashauri wananchi wenye malalamiko yenye mwelekeo wa kisheria kuyapeleka mahakamani ili yatatuliwe kwa mujibu wa sheria, akimshauri moja kwa moja mwananchi aitwaye Faraji kupeleka shauri lake mahakamani kwa kuwa linahusu madai.

“Ni utaratibu mzuri kuwasikiliza wananchi, lakini malalamiko yenye asili ya kisheria lazima yafikishwe mahakamani kwa ajili ya hatua za kisheria,” amesema Sendiga.

Katika hatua nyingine, amepokea barua za malalamiko kutoka kwa wananchi na kuzihusisha taasisi na idara zinazohusika ili kutoa majibu na ufumbuzi. 

Amewataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi na watendaji wa serikali kuhakikisha wanawajibika ipasavyo katika kuwasikiliza na kutatua kero za wananchi katika maeneo yao.

Vilevile, RC Sendiga amesema ni muhimu wazee kushirikishwa katika mabaraza ya kusikiliza kero za wananchi, akibainisha kuwa busara na hekima zao ni nyenzo muhimu katika kupata suluhisho la migogoro.

Baraza hilo maalum limehudhuriwa na wakuu wa idara za serikali, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala wa wilaya pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali.

 

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi