Na Timothy Itembe, Tarime
WANANCHI na wapiga kura wa Jimbo la Tarime Mjini wametakiwa kuwapigia kura wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana kupitia ushirikiano wa viongozi kutoka ngazi ya chini hadi ya juu.
Wito huo umetolewa na mgombea udiwani wa Kata ya Kenyamanyori, John Matiko, katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana, ambapo alisisitiza kuwa kwa kumchagua yeye pamoja na mgombea ubunge wa jimbo hilo, Esther Matiko, wapiga kura watakuwa wameweka msingi wa kushirikiana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo.
"Matiko ukijumlisha Matiko unapata Suluhu," alisema John Matiko, akimaanisha kuwa endapo yeye na Esther Matiko watapewa ridhaa ya uongozi, watafanya kazi kwa karibu na Rais Samia katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Matiko alitaja changamoto kadhaa zinazowakabili wakazi wa Kenyamanyori, ikiwemo miundombinu mibovu ya shule ya msingi Machori, hali duni ya barabara, na kutofika kwa fedha za makusanyo ya makapi ya dhahabu kutoka mgodi wa Kederi kwa wananchi wa kata hiyo.
"Nitumie nafasi hii kuwasilisha rasmi kero hizi kwa mbunge ajaye, Esther Matiko. Tunaimani kuwa kwa ushirikiano na viongozi wa juu, matatizo haya yatapatiwa ufumbuzi," alieleza Matiko.
Kwa upande wake, Esther Matiko, mgombea ubunge wa Tarime Mjini, alithibitisha kuwa kero hizo zimeainishwa kwenye ilani yake ya uchaguzi kwa kipindi cha 2025–2030, na ameahidi kuzifanyia kazi endapo atachaguliwa kuwa mbunge.
"Nitashirikiana kwa karibu na diwani wa kata hii pamoja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha ilani ya chama chetu inatekelezwa kikamilifu," alisema Esther Matiko.
Esther aliwataka wananchi kuwapigia kura wagombea wote wa CCM, kuanzia ngazi ya urais, ubunge, hadi udiwani, ili kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa ilani kwa mafanikio.
“Wapigakura wakinipa kura Oktoba 29, wanapaswa pia kunikumbusha ahadi ninazotoa wakati wa kampeni hizi ili nizitekeleze kwa uwazi na uwajibikaji,” alisisitiza.
Kwa niaba ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, Bwireri Motatiro aliwapongeza wagombea wa CCM kwa kuelewa na kugusa matatizo ya wananchi, na akawataka wapiga kura kuwapa kura zote siku ya uchaguzi.
