Katika mkutano uliofanyika septemba 29,2025 katika Kijiji cha Endanachan, Kata ya Ayasanda, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo, amesema chama hicho kimefanikiwa kutekeleza ahadi nyingi kupitia ilani ya miaka mitano iliyopita na sasa kinaomba tena ridhaa ya wananchi ili kuendeleza jitihada hizo.
Sillo amebainisha kuwa katika kipindi kipya cha 2025–2030, serikali itashughulikia kwa haraka changamoto kubwa za wananchi ikiwemo maji, barabara na umeme kwenye vitongoji ambavyo bado havijafikiwa.
“Serikali ilitoa shilingi bilioni 3.4 kugharamia elimu bila malipo, kila kijiji kufikiwa na umeme na sasa ni zamu ya vitongoji. Hakuna anayemaliza changamoto zote mara moja, ni hatua kwa hatua,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa UWT Wilaya ya Babati Vijijini, Tupilike Kabejela, ametangaza kuwa Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, atafanya mkutano wa kampeni Oktoba 3, mkoani Manyara, katika Kata ya Magugu akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Babati Vijijini, Jackson Haibey, amewataka wananchi kuhakikisha wanajitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu ifikapo Oktoba 29.
“Mabalozi wa nyumba kumi wahakikishe wanawakumbusha wananchi wajibu wao wa kidemokrasia,” alisisitiza.

Akizungumzia maendeleo yaliyopatikana, Mgombea Udiwani wa Kata ya Ayasanda, Yahaya Loya, amesema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kata hiyo imepokea miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 1.794, ikiwemo sekta ya afya (milioni 754.5), elimu ya msingi (milioni 81), elimu ya sekondari (milioni 138), ujenzi wa bweni la wasichana na bwalo la chakula katika Chuo cha VETA Ghorowa (milioni 367), barabara (milioni 380) na miradi ya maji (milioni 40).
Hata hivyo, Loya alikiri kuwa changamoto kubwa inayowakabili wananchi ni tatizo la maji, hususan Kijiji cha Endanachan ambacho kwa zaidi ya miaka 30 hakijawahi kuwa na huduma ya maji safi na salama.

Aidha, amebainisha changamoto za barabara ikiwemo Bonga–Endanachan, Endanachan–Gidas, Endanachan–Ayasanda na Endanachan–Pongay ambazo zinahitaji maboresho makubwa.
Kuhusu umeme, amesema ni vitongoji vitano pekee kati ya 11 vilivyopo vilivyoweza kufikiwa na huduma hiyo.
Pia ametaja changamoto ya makazi kwa watumishi wa afya katika Kituo cha Afya Ayasanda ambapo watoa huduma wanalazimika kuondoka saa tisa alasiri kutokana na ukosefu wa nyumba za madaktari.
Mkutano huo ulihudhuriwa na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Endanachan waliopokea kwa shangwe ujumbe wa wagombea na viongozi wa CCM.
